Thursday, May 31, 2012

HOFU ya kumpoteza mchezaji wake wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi, imeifanya klabu ya Simba kumweka sokoni kwa dau la sh bil. 2.
Simba itakuwa imeweka dau hilo kama wigo wa kumzuia kuondoka, kwani hakuna timu itakayoweza kutoa kiasi hicho cha fedha.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema mbali ya kiasi hicho, kuna masharti mengine kwa klabu itakayomtaka Okwi.

Kamwaga alisema sharti jingine ni kuweka bayana mshahara wa nyota huyo ili kumwepusha na dhiki ya maisha.
Sharti jingine, ni muhimu kwa klabu husika kuwa na uongozi imara ili nyota huyo asipate dhiki inayoweza kusababishwa na matatizo ya kiuongozi.

“Hayo ndiyo masharti kwa timu ambayo itakuwa inamhitaji Okwi, hatutakuwa kikwazo kwa klabu itakayokidhi vigezo hivi muhimu kwa maslahi ya mchezaji,” alisema Kamwaga.
Kamwaga alisema, wameweka bayana hilo kutokana na Okwi kuwindwa na klabu nyingi za ndani na nje ya nchi, ikiwemo Austria.

Alisema, kupitia mtandao klabu moja ya huko imeonesha kumtaka Okwi, hivyo wamewapatia masharti hayo muhimu kama kweli wanamtaka.
Kamwaga alisema, kama kutakuwa na klabu itakayoridhia masharti hayo iwe ndani au nje ya nchi, wao Simba hawatakuwa kikwazo.

CHANZO CHA HABARI: TANZANIA DAIMA na na Clescencia Tryphone

0 comments:

Post a Comment