Thursday, May 10, 2012

Msanii nyota wa filamu anayesumbuliwa na uvimbe tumboni, Juma Kilowoko `Sajuki'`
Safari ya msanii nyota wa filamu anayesumbuliwa na uvimbe tumboni, Juma Kilowoko 'Sajuki' ya kwenda nchini India kwa ajili  ya matibabu imeiva, baada ya wasamaria wema kumchangia kiasi cha Sh. milioni 16.
Japo fedha hizo ni pungufu ya Sh. milioni 9 ya fedha zote zilizokuwa zikihitajika kwa ajili ya safari ya msanii huyo kwenda nchini humo kutibiwa, lakini mkewe Wastara Juma ameshukuru kwa sababu inamwezesha mumewe kusafiri.
Akihojiwa na kituo kimoja cha redio, Wastara, alisema anawashukuru watu wote waliofanikisha kupatikana kwa fedha hizo pamoja na tiketi tatu za ndege za kumsafirisha mgonjwa, yeye na kaka wa Sajuki kwenye matibabu hayo.
"Kwa kweli nawashukuru watu wote waliojitolea kwa hali na mali kumsaidia mume wangu kwani nimefanikiwa kupata Sh. milioni 16 kati ya Sh. milioni 25 zilizokuwa zikihitajika," alisema.
Aliongeza kutokana na kupatikana kwa fedha hizo huenda wakaondoka nchini kwenda India kwenye matibabu kati ya Jumapili au Jumatatu ijayo.
"Nadhani kati ya Jumatatu au Jumapili ijayo tunaweza kusafiri ambapo mbali na Sajuki mwenyewe, kwenye msafara nitakuwepo na mimi na kaka wa Sajuki," alisema.
Hata hivyo Wastara alinukuliwa akilia na watu waliomliza kiasi cha Sh. 800,000 katika akaunti yake ya simu iliyokuwa ikitumiwa kuchangishia fedha hizo, ingawa anaendelea kuzifuatilia katika makao makuu ya mtandao huo wa simu za mikononi.

CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment