Wednesday, May 30, 2012

KESI ya msanii wa filamu Elizabeth Michael ‘Lulu’ (17), jana ilipigwa kalenda hadi Juni 11 mwaka huu kwa ajili ya maombi yake kuhusiana na uhalali wa umri wake yatakapotolewa uamuzi.
Jaji wa Mahakama Kuu, Dk. Fauz Twaib, anayesikiliza shauri hilo, alisema kutokana na utetezi kuwa mrefu, hana budi kupata muda ili aweze kuupitia na kuutolea uamuzi Juni 11 katika mahakama hiyo.

Mawakili wanne, Jacqueline Dimelo, Kennedy Fungamtama, Fulgency Massawe na Michael Kibatala ambao wanamtetea Lulu, wameiomba Mahakama hiyo kuchunguza umri wa Lulu au watoe idhini kwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufanya hivyo.

Hata hivyo, hali ilikuwa ya utulivu mahakamani hapo, tofauti na ilivyozoeleka mwanzoni mwa kesi hiyo ilivyoanza kusikilizwa, ambako pia mtuhumiwa alikuwa katika hali ya kawaida na kuwa na sura yenye tabasamu na kuweza kupeana ishara ya salamu na baba yake mzazi aliyefika kusiliza kesi ya binti yake.

Mara kwa mara, Lulu alikuwa akipepesa macho kila kona ndani ya mahakama hiyo na hata kuwaangalia watu wachache waliokuwemo ndani.
Mawakili wa Lulu, wanadai mteja wao ana miaka chini ya 18 hivyo shauri lake linapaswa kuendeshwa katika mahakama ya watoto.
Lulu anakabiliwa na tuhuma za kusababisha kifo cha aliyekuwa msanii mwenzake nyota wa filamu hapa nchini, Steven Kanumba, aliyefariki Aprili 7 mwaka huu nyumbani kwake Sinza Vatican jijini Dar es Salaam.

CHANZO CHA HABARI : Tanzania Daima http://www.freemedia.co.tz

0 comments:

Post a Comment