Wednesday, May 30, 2012

NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla amejitoa katika Kamati ya Fedha ya klabu ya Simba na kuanzia sasa atakuwa akizisaidia timu zote hapa nchini.
Makalla alibainisha hayo juzi, katika sherehe za klabu hiyo kujipongeza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara zilizofanyika ukumbi wa Dar Live Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Makalla, alisema, sababu ya kujitoa ni kutokana na wadhifu mkubwa alionao kwa sasa.

“Mimi nilikuwa ni mmoja wa viongozi waliokuwa katika Kamati ya Simba na kuchangia mafanikio haya ambayo Simba imeyapata, lakini kwa sasa kwa kuwa ni waziri, jukumu langu ni kusaidia timu zote nchini bila ya kujali Simba wala timu yoyote,” alisema Makalla.
Aliuasa uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi, kutoridhika na mafanikio hayo na kuwaomba kuzidi kupigana kufa na kupona ili kuendeleza hali ya mafanikio ndani ya klabu hiyo na kujipanga ili kufanya vizuri zaidi.
Alisema ana imani kubwa klabu ya Simba ina uwezo mkubwa wa kujenga uwanja mzuri wa kisasa kutokana na ukongwe ambao inayo.

Katika sherehe hizo, Makalla akimkabidhi nahodha wa Simba, Juma Kaseja, tuzo na medali maalumu kwa ajili ya aliyekuwa mchezaji wa timu hiyo, marehemu Patrick Mafisango aliyefariki hivi karibuni kwa ajali ya gari, ambapo nahodha huyo alishindwa kujizuia na kuangua kilio na kuwafanya baadhi ya wachezaji wenzake, mashabiki na wapenzi kuanza kumwaga machozi.

Kabla ya kutolewa kwa tuzo hiyo, ulipigwa muziki wa ‘Kazi yake Mola Haina Makosa’ wa Msanii Madee kumkumbuka Mafisango na mara baada ya wimbo huo kumalizika, shughuli zote ukumbini hapo zilisimama kwa dakika moja na watu wote walisimama na kumwombea mchezaji huyo.
Naye Meneja wa Global Publishers Limited, Abdallah Mrisho, alikabidhi sh milioni 3 kwa Kaseja, kama zawadi yao kwa wachezaji na benchi la ufundi ikiwa ni pongezi kwa kazi nzuri waliyoifanya katika msimu uliopita wa 2011/12 hadi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
Sherehe hizo zilipambwa na wanamuziki na bendi mbalimbali hapa nchini, ikiwemo Msondo, Mshauzi Classic, Young D.
CHANZO CHA HABARI:http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=36432

0 comments:

Post a Comment