Thursday, May 31, 2012

Edward Lowassa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo Nje, Ulinzi na Usalama imeitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kutoa maelezo kuhusu taarifa yake kwamba, kuna askari 700 wa Jeshi la Polisi na 248 wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliobainika kila mmoja kutumia cheti kimoja cha elimu na mtu mwingine.

Taarifa hiyo ya Nida ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wake, Dickson Maimu, alipokutana na wahariri na waandishi wa habari, jijini Dara es Salaam, Mei 14, mwaka huu, kueleza sababu za kuchelewa kutoa vitambulisho vya taifa vilivyotarajiwa kuanza kutolewa mwanzoni mwa mwezi huu.

Kauli ya kuitaka Nida kutoa maelezo hayo, ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Edward Lowassa, wakati kamati yake ilipotembelea makao makuu ya mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam jana.

Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM), alisema licha ya mkurugenzi mkuu wa Nida kukanusha taarifa hiyo baadaye, maneno aliyotumia wakati anakanusha, hayafanani na yale aliyotumia wakati anatoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari.

“Jambo la tatu linahusu maneno yaliyotolewa na vyombo vya habari kuhusu polisi na JWTZ. Ulikanusha lakini maneno (uliyotumia kukanusha) hayafanani na ya kwanza,” alisema Lowassa.

Siku chache baada ya kutoa taarifa hiyo na kutangazwa na vyombo vya habari, Nida ilitoa taarifa ikikanusha madai ya kubaini vyeti feki katika JWTZ na Polisi.

Katika tamko hilo, Nida ilisisitiza kuwa wao hawana uwezo wala mamlaka ya kubaini vyeti feki na kwamba, taarifa zilizotelewa na kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari zilikuwa ni upotoshaji.

Hata hivyo, Lowassa alimpa Mkurugenzi Mkuu huyo wa Nida uhuru wa kuchagua kutoa maelezo hayo ama kwa kamati yake au mbele ya waandishi wa habari pia.

Akijibu hoja hiyo, Maimu alisema taarifa kuhusu suala hilo tayari alikwishaieleza kwa waandishi wa habari, hivyo akaomba kwa sasa aitoe kwa kamati hiyo.

Awali, akichangia mjadala kuhusu mradi huo, Mbunge wa Uzini (CCM), Muhammed Seif Khatib, alipongeza kwa kufanikiwa kutekelezwa hivi sasa tofauti na huko nyuma.

Alisema licha ya kuwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na pia baadhi ya mawaziri wengine waliowahi kuongoza wizara hiyo kabla na baada yake, walishindwa kufanikisha mradi huo kutekelezwa kutokana na kuwapo fitina nyingi.

Kauli hiyo ya Khatib iliungwa mkono na Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), John Chiligati, ambaye naye alikiri kipindi alichoongoza wizara hiyo hakikuwezesha mradi huo kutekelezwa.

Chiligati alisema sababu kubwa ni kuwa mradi huo unahusisha fedha nyingi, hivyo kila aliyekuwa akitaka kupata zabuni ya kuutekeleza, alipoikosa, alianzisha fitina, ikiwamo kukimbilia mahakamani na kuukwamisha.

Hata hivyo, alisema vipindi hivyo vya fitina vimepita na kusema kinachotakiwa kwa sasa ni kufanya kazi ili kufanikisha mradi huo.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji wa Vitambulisho, Joseph Makani, aliieleza kamati hiyo kuwa usajili wa watu mkoani Dar es Salaam litaanza rasmi mwezi ujao, baada ya mafunzo ya jinsi ya kuendesha zoezi hilo kwa watendaji wote wa mkoa huo na halmashauri zake zote.


  CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment