Thursday, May 31, 2012




















Mussa Juma, Arusha.
RAIS Jakaya Kikwete leo anatarajiwa kufungua rasmi, mkutano wa mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika(AfDB) mjini Arusha.

Taarifa iliyotolewa jana kwa Vyombo vya habari katika mkutano wa benki hiyo, unaoendelea mjini humo, imeeleza kuwa ufunguzi huo utafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

Marais mbalimbali wa nchi za Afrika walitarajiwa kuwasili jana kuhudhuria mkutano huo, ambao vikao vyake, vilianza tangu Mei 28 mwaka huu, katika hoteli tofauti.


Akizungumzia na Mwananchi jana, Mkuu wa Mkoa Arusha, Magesa Mulongo alisema tayari Rais Kikwete aliwasili jana mjini humo ambapo marais wengine  walitarajiwa kuanzaa kuwasili jana jioni.

Alitoa wito kwa wakazi wa Arusha, kudumisha amani katika kipindi hiki ambacho kuna ugeni mkubwa wa watu.

"Ninachoomba mimi ni amani tu, kwani mji umefurika , hoteli zimejaa, kila mtu anafanya biashara"alisema Mulongo.

Katika mkutano huo wa AfDB mikataba mbalimbali imekuwa ikisainiwa baina ya nchi wanachama na taasisi za fedha, ambapo pia mada mbali mbali zimekuwa zikitolewa na kujadiliwa.

Katika vikao vya jana, hali ya amani nchini Sudani na Somalia ilijadiliwa na wito ulitolewa kuongezwa jitihada za kutafutwa amani ya kudumu.
Wakati huohuo, Pamela Chilongola anaripoti kuwa
Tanzania imeunga mkono jitihada ya Ivory Coast kurudisha makao makuu ya AfDB, katika mji wake mkuu Abidjan.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilisema Rais Jakaya Kikwete alimweleza Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast hatua hiyo wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika jana mkoani Arusha.

Rais Kikwete alisema Tanzania inaunga mkono jitihada za kurudisha makao makuu hayo mjini  Abidjan, yalipokuwa makao makuu kabla ya kutokea vurugu za kisiasa nchini humo.

CHANZO CHA HABARI:GAZETI LA MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment