Thursday, April 26, 2012


NI EZEKIEL MAIGE, ADAI ALIINUNUA KWA DOLA 410,000, LEMBELI APINGA, ASEMA ALIINUNUA KWA DOLA 700,000 TASLIMU
SIKU chache baada ya gazeti hili kuripoti taarifa za uchunguzi kwamba kuna mawaziri wawili ambao wamenunua nyumba mbili zenye thamani ya Sh1.8 bilioni, mmoja wa mawaziri hao, Ezekiel Maige wa Maliasili na Utalii ameibuka na kukiri.Maige aliliambia gazeti hili jana kuwa nyumba yake hiyo iliyoko Mbezi Beach, Dar es Salaam, ameinunua kwa Dola za Marekani 410,000 (takriban Sh656 milioni) ambazo anadai kuwa ni mkopo kutoka Benki ya CRDB.

Hata hivyo, wakati Waziri Maige akieleza kuwa nyumba hiyo ina thamani hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli amedai kuwa taarifa alizonazo ni kwamba ilinunuliwa kwa fedha taslimu Dola 700,000 za Marekani (takriban Sh1.1 bilioni).

Awali, habari zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa Waziri Maige alinunua nyumba hiyo kutoka kwa Kampuni ya Savana Real Estate.

Mmoja wa madalali wanaouza nyumba za kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Athuman (Ustadhi) alilithibitishia gazeti hili kwamba Waziri Maige amenunua nyumba moja kati ya nne zilizoko sokoni.

Hata hivyo, dalali huyo hakutaka kueleza alinunua nyumba hiyo lini na kwa gharama gani baada ya kueleza kuwa yeye si msemaji wa kampuni hiyo.

“Nyumba zipo nne na mbili zimeshauzwa. Maige kanunua nyumba moja. Nyumba nyingine mbili bado hazijauzwa na kwa sasa tunamalizia kuziwekea milango na bustani,” alisema Athuman.

Akizungumza na gazeti hili jana, Waziri Maige alisema hakununua nyumba hiyo kwa Dola 700,000 kama inavyodaiwa, bali alinunua kwa Dola za Marekani 410,000.
Mbali ya kukiri, alifafanua jinsi alivyoinunua na kuonyesha nyaraka mbalimbali huku akieleza kuwa sehemu ya fedha alizonunulia, zilikuwa za mkopo kutoka Benki ya CRDB.

Alisema mwaka 2005 alipoanza kuwa mbunge alipata mkopo na yeye na wenzake watatu, waliunda kampuni ya kusafirisha mzigo ya Splendid Logistic na kuanza kununua magari matatu na baadaye magari hayo yaliongezeka na kufikia saba.

Waziri wa Maliasili na Utalii,Ezekiel Maige
Alisema Septemba, 2010 mwenzao mmoja alijitoa katika kampuni hiyo na hivyo wakaamua kugawana mali kwa kuzingatia mtaji wa kampuni. Alipata magari mawili na mwenzake manne na kuongeza kuwa gari moja kati ya hayo saba lilipata ajali.

Alisema baada ya hapo aliamua kuanzisha kampuni nyingine ya kusafirisha mizigo ambayo inaendeshwa na mke wake... “Kampuni hiyo inaitwa Mem Logistic na ina magari mawili.”

Alisema magari hayo aliyakodisha kwa kampuni nyingine ya Bravo Logistic ambayo kila mwezi inamlipa Dola 20,000.

Alisema alipochaguliwa tena kuwa mbunge mwaka 2010 aliamua kutoongeza magari katika kampuni yake na kuanza kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.

“Baada ya uchaguzi nilichukua mkopo wa Sh200 milioni katika Benki ya CRDB, baadaye Ofisi ya Bunge ilinikopesha Sh90 milioni kwa ajili ya kununua gari, fedha hizo zote nilizichukua na kuzihifadhi,” alisema Maige.

“Hizo fedha nilikaa nazo nikawa nataka kujenga nyumba baadaye nikaona nitafute nyumba ya kununua tu. Baadaye dada yangu, Angelina Ngarura ambaye ana kampuni ya kuuza matrekta, Dar es Salaam alinifuata na kuniomba fedha hizo kwa ajili ya kuzizungusha na tukakubaliana kuwa atakuwa akilipa riba ndogo kwa makubaliano kwamba siku yoyote nikizihitaji nitazichukua,” alisema.

Alisema ndipo alipopata nyumba iliyokuwa ikiuzwa Dola 450,000 lakini alikubaliana na muuzaji na kuuziwa kwa Dola 410,000.

Alisema katika ununuzi huo, hakuwa na kiasi hicho cha fedha kwani nyingine zilikuwa katika mzunguko katika kampuni ya dada yake na hivyo kuamua kwenda kukopa Dola 200,000 katika CRDB.

Alisema baada ya kupewa fedha hizo za mkopo, hati ya nyumba hiyo ilibaki benki kwa makubaliano kwamba akishindwa kulipa, benki itaichukua.

“Tuliingia mkataba na CRDB kulipia nyumba ile kwa miaka minne na mpaka sasa hivi nalipia Dola 5,127 kila mwezi, haya yote yapo kwa Kamishna wa Maadili,” alisema Maige.

Huku akionyesha mikataba ya ununuzi wa nyumba hiyo, nyaraka za mkopo wa benki, Maige alisema awali, alikuwa na magari mawili ambayo aliamua kuyauza na kununua gari nyingine aina ya BMW kwa Sh70 milioni.

Alidai kwamba kama kuna mali kinyume na hizo yuko tayari kuapa hata kwa Biblia Takatifu na kusisitiza kuwa hivi sasa kuna mapambano ya kisiasa ndiyo maana shutuma dhidi yake zinaibuka kila kukicha.

“Ukisikia mali zangu tofauti na hizo ni uongo ndugu yangu na kwa mkopo niliochukua wakati nikiwa mbunge sina hela mpaka Juni 2015,” alisema na kuongeza:
“Nikijiuzulu ubunge leo hii maana yake ni kwamba itakuwa kazi kweli na sitaweza kulipa mkopo. Sijakopa kwa kivuli cha ubunge wangu, nimekopa kama Maige kwa sababu kiwango cha kukopa bungeni nimeshakimaliza.”

Maige alidai kuwa hivi sasa habari mbaya zinaibuka dhidi yake akidai kwamba kuna watu ambao hata hivyo, hakuwataja kwamba ndiyo wanaopanga mikakati ya kumhusisha na mambo mbalimbali ili aonekane si mwadilifu katika jamii.

Lembeli: Amenunua taslimu

Wakati Maige akisema alikopa fedha hizo benki, Lembeli alidai kwamba anazo taarifa kwamba waziri huyo alinunua nyumba hiyo kwa fedha taslimu.

“Nilianza kusikia na baadaye kuthibitishiwa. Kuna watu waliokuwa na nyaraka wakasema wana ushahidi kuwa nyumba hiyo ni ya mheshimiwa waziri,” alisema Lembeli na kuongeza:

“Baadaye nikasoma kwenye magazeti kwamba mawaziri wawili vijana, wamenunua nyumba za mabilioni, sasa kama watu wanasema sioni sababu ya kupuuza madai hayo.”

Lembeli alisema si kosa kwake na wengine kuamini taarifa hizo kwa kuwa watu waliompa walizitetea kwa ushahidi na waliamua kufuatilia suala hilo baada ya kukumbana na ukiritimba mwingi walipokuwa wakitafuta huduma wizarani.

“Usipowatendea watu haki, hakika watakufuatilia na mimi sina sababu ya kutilia shaka kauli ya watu hao kwamba nyumba hiyo ni ya Maige na imenunuliwa kwa Dola 700,000,” alisema.
CHANZO NI GAZETI LA MWANANCHI LA LEO 26/4/2012

0 comments:

Post a Comment