Thursday, July 25, 2013

Picture: 
Baobab oil, mafuta ya ubuyu WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema bado haitambui mbegu za ubuyu kuwa zinatoa mafuta ambayo ni tiba. Aidha imesema inatambua kuwa tiba kutokana na mti huo ni majani, magome na unga wa ubuyu.

Wizara pia imeitaka jamii kuwa macho na waganga wa tiba za asili na tiba mbadala ambao hawajasajiliwa kwa kuwa kama zilivyo dawa nyingine, tiba ya asili ina madhara yanayoweza kuleta matatizo makubwa katika maisha ya mtu kama haijapimwa na kuthibitishwa.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili na Tiba Mbadala wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Paulo Mhame aliyasema hayo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari katika semina ya siku moja kuhusu masuala ya tiba asili na tiba mbadala nchini.

Akizungumzia ubuyu, baada ya kuulizwa swali kama ni sahihi mafuta ya ubuyu kutumiwa kama tiba Dk Mhame alisema Serikali haitambui mafuta ya ubuyu kama tiba.

Alisema mti wa ubuyu unatumika kama tiba kwa baadhi ya mazao yake kuchanganywa na vitu vingine na kutoa dawa ikiwemo majani, magome yake na unga wa ubuyu wenyewe, lakini mpaka sasa hakuna taarifa ya kitaalamu kuhusu mafuta ya ubuyu kuwa dawa.

Dk Mhame alisema nchi za Magharibi zimekuwa zikinunua mafuta ya ubuyu kutoka Afrika kwa ajili ya kutengeneza vipodozi: “Nchi za Ulaya zimekuwa zikinunua mafuta ya ubuyu kutengeneza vipodozi, mtu mwenye miaka 90 anataka kuonekana ana miaka 60,” alifafanua Dk Mhame.

--- Gloria Tesha/HabariLeo

0 comments:

Post a Comment