Sunday, January 27, 2013

Jikabidhi kabisa kwa Mungu, atakutumia kutimiza mambo makuu kwa hali ambayo utaamini zaidi kwamba ni Upendo wake dhidi ya Udhaifu wako.
 – Mama Theresa
Siku ya Ukoma Duniani huadhimishwa Duniani kote kila Jumapili ya mwisho ya mwezi Januari. Huadhimishwa ili kuongeza Ufahamu wa Ugonjwa wa Ukoma (Leprosy/Hansen's Disease) .

Siku iliteuliwa ili kuwe ni Kumbukumbu ya Kifo cha Gandhi, Kiongozi wa India aliyetambua umuhimu wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma.

Ukoma ni moja ya magonjwa ya zamani Duniani. Ni ugonjwa sugu unaoambukizwa na vijidudu vya bakteria, unaathiri mfumo wa fahamu hasa neva za mikono, miguu na uso.

Kwa zaidi ya Miaka 50, kila Jumapili ya mwisho ya mwezi Januari, maelfu ya watu Duniani kote wameacha kuwakumbuka wale walioathiriwa na Ukoma.

Mwaka 1953, M. Raoul Follereau wa Ufaransa alianzisha Siku ya Ukoma Duniani kwa mara ya kwanza, ili kuleta hamasa kuwaangalia na kuwezesha misaada kwa mamilioni ya watu waliothiriwa na Ukoma Duniani kote katika zama hizi. Kwa miaka mingi, uangalifu umeongezeka na zaidi ya nchi 100 hushiriki kwenye siku ya Ukoma Duniani, kila Jumapili ya mwisho ya  mwezi Januari.

Kwa karne nyingi katika nchi nyingi, Ukoma umefanya watu walioathiriwa nao kutengwa na jamii zao kwakuwa haukuwa na dawa kwa ajili ya matibabu. Watu walioathiriwa na Ukoma iliwabidi kuishi na ulemavu unaosababishwa na Ukoma.

Siku ya Ukoma inasaidia kusimulia hadithi kwa watu wasiojua kuwa Ukoma bado upo ila sasa unaweza kutibiwa. Siku hii husaidia pia kukusanya pesa kwa ajili ya matibabu ya watu wenye Ukoma na utunzaji wao.

Tuungane kuadhimisha siku ya Ukoma Duniani, Jumapili ya Januari 27, 2013 na tusimame kwa ajili ya wale wanaoteswa na unyanyapaa kila siku. Sisi ni ndugu, ni mwili mmoja, tusaidiane na kujaliana.

KUHUSU UKOMA
Ukoma ni ugonjwa ambao umekuwapo kwa karne nyingi sana tangu kipindi cha biblia. Ni ugonjwa unasababisha majeraha katika ngozi, huharibu mfumo wa neva na kudhoofisha mwili, matatizo huwa zaidi kadili muda unavyokwenda.

VISABABISHI
Ukoma husababishwa na bakteria waitwao Mycobacterium leprae. Bakteria hawa hukaa muda mrefu katika mwili kabla ya kutokeza dalili za ugonjwa, kitu kinachosababisha ugonjwa ugumu wa kutojua ni wapi na ni lini mtu alipopata maumbukizi. Watoto wako katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.

MAMBO HATARISHI
Maeneo yenye ukoma sana huwa na hatari zaidi. Vitu vifuatavyo huongeza hatari ya kuambukizwa mfano kulala kitanda kimoja na mgonjwa wa ukoma asiyetibiwa, kutumia maji yaliyotumiwa na mgonjwa wa ukoma na ukosefu wa lishe bora au ugonjwa wowote unaoshusha kinga ya mwili.

JINSI UNAVYOAMBUKIZWA
Wanasayansi bado hawajagundua jinsi hasa ukoma unavyoambikizwa. Wengi wao husema bakteria wa ukoma husambaa kutoka kwa mtu mmoja mwenye maambukizi hadi kwa mwingine kwa njia ya hewa. Haijagundulika kama unaweza enea kwa njia ya ngono. Uchunguzi umebaini pia ukoma unaweza kuambukizwa kwa binadamu na mnyama mdogo kama sungura anayejulikana kitaalamu kama armadillos, anayepatikana sana Amerika ya kati na Kusini.

DALILI:
-Kupasuka kwa ngozi au kuwa na mabaka kwenye ngozi. Mipasuko ya ngozi huwa na rangi iliyofifia zaidi kuliko rangi ya kawaida ya ngozi ya mwili wako. Mipasuko hupunguza nguvu ya kuhisi mguso, joto au maumivu. Mipasuko haiponi haraka, inaweza kuchukua wiki kadhaa hadi miezi.
-Mwili kuishia nguvu.
-Mwili kufa ganzi hasa kwenye viganja, mikono na miguu.

VIPIMO:
Wataalamu wa afya hufanya uchunguzi kwenye maabara kwa kuchukua mpasuko wa ngozi au kipande kidogo cha nyama cha mtu anaedhaniwa kuwa na ugonjwa wa ukoma au kwa mgonjwa wa ukoma ili kujua ni aina ipi ya ukoma inayomsumbua.

MATIBABU:
Tiba inapatikana bure kwenye hospitali zote za serikali ambapo wagonjwa hupewa dawa za kuua bakteria na dawa za kuzuia na kupunguza kuvimba kwa mwili.

Serikali pia hugharamia viatu maalumu kwa wagonjwa wa ukoma ili kuzuia athari na kupunguza ulemavu utokanao na kuharibiwa kwa mishipa ya fahamu, huduma za marekebisho ambazo ni pamoja na huduma za upasuaji, viungo vya bandia, magongo na viti mwendo.

Kugundua ugonjwa mapema ni muhimu sana. Matibabu ya mapema huzuia athari za ukoma, na kuzuia mtu mwenye ukoma kusambaza kwa wengine na kumsaidia mtu kuwa na maisha ya kawaida.

ATHARI ZA UKOMA:
Mwili kuwa katika umbo la ajabu mfano miguu kuvimba sana, mwili kuchoka, tatizo la kudumu la neva kwenye mikono na miguu, kupoteza nguvu ya kuhisi vitu. Watu wenye tatizo la kudumu la ukoma wanaweza poteza uwezo wa kutumia mikono au miguu yao kutokana na majeraha kwasababu wanakosa hisia ya maeneo hayo mfano wanaweza kuungua moto bila ya wao kujua.

MUDA GANI SAHIHI KUFIKA KWENYE HUDUMA ZA AFYA:
Fika kwenye huduma za afya pale unapopata dalili za ukoma hasa kama umewahi kugusana na mtu mwenye ukoma. Dalili muhimu ni baka au mabaka kwenye ngozi yasiyo na hisia ya mguso ambayo huambatana na ganzi kwenye mikono na miguu.

KUZUIA:
Kujikinga na ukoma kunahusisha kutogusana na mtu mwenye ukoma ambaye hakutibiwa. Pia watu walio katika matibabu kwa muda mrefu hawawezi kusambaza Ukoma

0 comments:

Post a Comment