Thursday, November 1, 2012

Nukuu ya gazeti la NIPASHE

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amesema shehena na makontena mawili ya meno ya tembo yaliyokamatwa Hong Kong, yatachunguzwa kwa kutumia vinasaba (DNA) ili kubaini kama asili yake ni Tanzania.

Aidha, amesema maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wale waliokuwa zamu siku shehena hiyo ikipitishwa bandarini Dar es Salaam kwenda Hong Kong, wanachunguzwa ili kubaini ukweli.

Alisema hayo wakati akifanya majumuisho ya hoja za wabunge waliokuwa wakijadili maazimio mawili ya Bunge kuhusu marekebisho ya mpaka na upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe na lile la kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane, “Hatuna uhakika bado kama meno yaliyokamatwa huko Hong Kong yana asili ya Tanzania au yalikuwa yakipitishwa nchini mwetu…tunafanya mazungumzo na balozi wetu kule China kuhusu suala hilo,” alisema.

Alisema taarifa ambazo zimekwishapatikana zinaonyesha kwamba kontena moja linatokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kontena lingine bado halijaeleweka wazi kwamba linatokea Tanzania au la, na ndio maana uchunguzi utahusisha vipimo vya DNA ili kujua asili ya meno hayo.

Oktoba 16, mwaka huu, maofisa usalama wa Hong Kong waliyakamata makontena mawili yaliyokuwa yamesheheni meno ya tembo yenye thamani ya dola za Marekani milioni 3.4. Hata hivyo, kontena moja kati ya hayo lenye thamani ya dola za Marekani milioni 1.7 linadaiwa kuwa linatokea Tanzania. Kama hiyo haikutosha, shehena ya meno ya tembo ilikamatwa bandarini Dar es Salaam Jumapili iliyopita na hali ambayo inaonyesha kasi ya kuuwa kwa tembo ni kubwa.

Mapema katika mchango wake binafsi, mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa, alisema kuongeza mipaka ya hifadhi ni suala zuri lakini serikali inawajibu wa kulinda hifadhi hizo.

Alizungumzia tukio la hivi karibuni la kukamatwa kwa meno ya tembo huko Hong Kong na bandarini Dar es Salaam yanaashiria kwamba tembo waliopo kwenye hifadhi wanauawa, “Hii inaonyesha jinsi gani tembo wetu wanavyoteketea,” alisema na kuongeza, “sifurahishwi sana kuona tembo wetu wanakufa.”

Nukuu ya gazeti la HABARI LEO

SERIKALI imesema inafuatilia kwa karibu taarifa za kupatikana makontena mawili ya meno ya tembo yaliyokamatwa Hong Kong yanayosadikiwa yametokea Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki alitoa maelezo hayo wakati akifanya majumuisho ya Azimio la Marekebisho ya Mpaka na upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe na kumjibu Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (CHADEMA) ambaye katika mchango wake, aligusia kukamatwa kwa meno hayo China.

“Meno ya tembo kama 150 kukamatwa China na hivi juzi wengine kukamatwa nchini, kunaonesha jinsi tembo wanavyoteketea, kukamatwa wahalifu haisaidii kama kuzuia tembo wasiuawe, tuweke mipango kuhakikisha wanyama wanalindwa,” alisema Msigwa.

Katika majibu yake, Balozi Kagasheki alisema kwa sasa Serikali kupitia Balozi wake wa China, Philip Marmo, Mkuu wa Polisi, Inspekta Jenerali Saidi Mwema na polisi wake na yeye na maofisa wizarani kwake wanalifuatilia suala hilo kwa karibu ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Alisema, “Leo (jana) tu nimekuwa nikizungumza na Balozi wetu China na mimi na IGP na system yake ya polisi tunalifuatilia hili kwa undani ili tujue kontena hilo lilipitaje nchini kwenda China na siku hiyo pale custom (bandarini) nani alikuwepo zamu.”

Hata hivyo, alisema ripoti zilizokuwapo za Hong Kong zinaonesha utata kwani zinasema kontena moja lilitokea DRC na jingine Tanzania, lakini ripoti nyingine zinasema kontena hilo la pili halikutokea nchini, bali lilipitia likielekea Hong Kong.

Waziri alisema kutokana na utata huo, wanafuatilia kwa karibu ili kuujua ukweli na kuchukua hatua za kisheria kwa haraka; na kuongeza “pale wizarani watu tunafanya kazi tunaomba mtuamini tushughulikie vizuri.”

Makontena hayo mawili ya meno ya tembo yenye vipande 1,209 ya thamani ya zaidi ya Sh bilioni 2.5 yenye uzito wa paundi 8,000 yalikamatwa wiki mbili zilizopita katika Bandari ya Hong Kong baada ya kupata taarifa kutoka kwa maofisa wa forodha wa Jimbo la Guangdong, China.

Taarifa zinasema kontena linalosadikiwa kutoka nchini, lilikuwa na mabaki chakavu ya plastiki yaliyokuwa yakienda kuzalishwa upya na ndani yake yalikutwa meno yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1.7.

Katika tukio hilo, watu saba akiwamo mkazi mmoja wa Hong Kong wamekatwa wakiwa huko kutokana na kuhusishwa na kontena hizo za meno ya tembo.

0 comments:

Post a Comment