Friday, November 30, 2012

Lissu amkomalia JK

MNADHIMU wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, ameendelea kumwandama Rais Jakaya Kikwete, akisema baadhi ya majaji aliowateua hawana sifa, na kwamba viongozi wa serikali waliojitokeza kumpinga wameshindwa kujibu hoja.

Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana katika ofisi ndogo ya Bunge, Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), alisema kuwa alishatoa maelezo hayo hata katika Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi.

“Nilieleza jinsi rais alivyofanya uteuzi wa baadhi ya majaji pasipo kupata ushauri wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. Wamekuwa wakijibu kiujumla, mimi niliwataja kwa majina yao na hata hili nilieleza katika Kamati ya Ngwilizi ambayo taarifa yake haikuwekwa hadharani pasipo sababu za kueleweka,” alisema.

Alisema wanaotaka kujibu hoja zake wanapaswa kuweka hadharani orodha ya majina ya majaji waliopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kuanzia mwaka 2005 wakati Rais Kikwete alipoingia madarakani.

Lissu aliwataja baadhi ya watu waliowahi kujitokeza kumjibu kuwa ni Naibu wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki, ambaye alisema kuwa serikali ina taarifa hizo na itazifanyia kazi.

Alisema kuwa msimamo huo ulikubaliwa na waziri wake, Mathias Chikawe na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ambao kwa nyakati tofauti walisema kuwa, endapo serikali itachukua hatua ambazo alipendekeza watakuwa wanaingilia uhuru wa mahakama.

Wengine waliojitokeza kujibu hoja yake ni Jaji Mkuu, Othman Chande na Jaji Kiongozi, Faki Jundu ambao walisema kuwa tuhuma zilizotolewa bungeni si za kweli.

Pia Rais Kikwete naye alikaririwa hivi karibuni akiwa jijini Arusha ambapo bila kumtaja Lissu kwa jina, alisema kuwa majaji wanateuliwa kwa kufuata utaratibu na wana sifa zinazostahili.

Ni kutokana na kauli hizo, Lissu alifafanua kuwa, katika hoja zake alisema kuna baadhi ya majaji waliteuliwa bila kuwa na sifa maalumu kama zilivyobainishwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 109, kipengele cha 6, 7 na 8.

“Ibara hiyo ya 109 kipengele cha 6-8 kinasema; mtu anaweza kuwa Jaji iwapo tu ana shahada ya sheria kutoka katika chuo kinachotambuliwa kisheria, awe ameshakuwa hakimu, awe ameshakuwa wakili na kusajiliwa na sifa zote hizo ziambatane na utumishi wa miaka kumi mfululizo.

“Lakini sifa zote hizo lazima mtu anayeteuliwa kuwa Jaji awe nazo kwa miaka kumi mfululizo. Sasa badala ya kuzungumzia masuala hayo kwa ujumla jumla, ningependa wanaonijibu watamke wazi wazi Jaji Mbaruku Salumu Mbaruku alisoma chuo kipi na akapata shahada ya sheria iliyompa sifa ya kuwa jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar kabla ya kuteuliwa kuwa jaji wa Mahakama ya Rufaa hadi sasa,” alisema.

Alishangaa viongozi wanaojitokeza kumjibu akisema hata Katiba ya Zanzibar 94 (3) inasema; ili mtu achaguliwe kuwa jaji, ni lazima awe na shahada ya Chuo Kikuu.

“Huyu jaji ambaye anasoma sasa alipataje kuwa jaji kabla ya kuwa na shahada ambayo ndiyo sifa ya msingi?” alihoji.

Lissu aliwataja majaji wengine ambao wameteuliwa bila kuwa na sifa kuwa ni Fatuma Masengi, ambaye kwa mujibu wa Lissu alikuwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Singida na baadaye akawa Hakimu Mkazi kisha akaanza kujisomea Chuo Kikuu Huria na kuhitimu mwaka 2003 na kuteuliwa kuwa jaji mwaka 2006.

Alihoji kuwa kama katiba inaelekeza mtu awe jaji ni mpaka awe amekuwa hakimu kwa miaka 10, huyu alipataje kuwa jaji?

Majaji wengine waliotajwa ni Latifa Mansoor, ambaye pamoja na kuwa na shahada ya sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyotunukiwa 1993, lakini alifukuzwa kwa udanganyifu na ubadhirifu akiwa mfanyakazi katika Manispaa ya Ilala.

Kwamba baadaye alipoibuka mwaka 2008 aliteuliwa kuwa jaji wakati hajawahi kuwa wakili, na kwa kuwa alifukuzwa katika utumishi wa umma.

Lissu pia alimlalamikia Rais Kikwete kwa kutumia vibaya madaraka yake kwani anateua majaji wa mikataba, ambao wameshastaafu na kulipwa mafao yao.

Aliongeza kuwa, majaji wengine waliteuliwa na Rais wakiwa wagonjwa ili waweze kupata fursa ya kwenda kutibiwa nje ya nchi, ambapo alimtolea mfano Jaji Mwendwa Malecela kuwa tangu ateuliwe mwaka 2006 hajawahi kusikiliza kesi hata moja. Badala yake Lissu alidai kuwa jaji huyo huenda matibabu India tu.

Kufuatia utata huo, Lissu emeendelea kushikilia msimamo wake kuwa anakusudia kupeleka hoja binafsi bungeni ili Bunge liweze kuchunguza utendaji wa rais kuhusu uteuzi wa majaji.

Lissu alisema Bunge litaangalia kama rais ameteua majaji kwa mujibu wa katiba au ameikiuka, na kwamba yeye ana uhakika kuwa rais amekiuka katiba.

Chanzo: Tanzania Daima | Nov 29, 2012

0 comments:

Post a Comment