Wednesday, November 7, 2012

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu, amevunja ukimya na kuzungumza kwa mara ya kwanza akisema hakupewa fedha na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, wala hakutumia rushwa mtandao kumuangusha Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye.

Kauli hiyo ya Nagu imekuja wakati ambapo Sumaye anadai kuwa rushwa ya kimtandao iliyokigubika Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndiyo iliyomwangusha wilayani Hanang wakati akipambana na Dk. Nagu katika uchaguzi kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa.

Wakati kukiwa na taarifa kuwa kuna baadhi ya wanachama wameandika barua kwa Katibu Mkuu wa CCM, kutaka ushindi wake utenguliwe, Nagu akizungumza na gazeti hili jana katika mahojiano maalumu, alisema kuwa anamshangaa Sumaye kudai aliangushwa kwa rushwa.

Alisema hakupewa fedha na aliyekuwa Waziri Mkuu, Lowassa, kwa ajili ya kumuangusha Sumaye na kwamba wananchi wa Hanang walimchagua kwa ridhaa yao. Nagu alisema wanaosema kuwa alitumia rushwa, wana mfumo dume kwa sababu hawaamini kama mwanamke anaweza kushinda bila rushwa.

“Huu ni mfumo dume, usiotambua uwezo wa mama unatawala. Tushirikiane kuutokomeza,” alisema Dk. Nagu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hanang.

Dk. Nagu ambaye hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa undani kwa sababu Sumaye alikuwa bosi wake wakati akiwa Waziri Mkuu, alisema alinyanyasika sana wakati wa uchaguzi huo wa Hanang.

Alisema ilifika mahala watu aliokuwa akipingana nao walikuwa wakisema wakati wa mwanamke kuchukua nafasi hiyo umekwisha na kwamba amuachie mwanaume aongoze.

Alisisitiza kuwa, yeye kwa upande wake hakutoa rushwa wala hakufadhiliwa na mtu yeyote na kuwashutumu wapinzani wake kuwa ndio waliotumia rushwa kuhakikisha wanamuangusha, lakini walishindwa.

“Kama nilitoa rushwa, TAKUKURU wapo, kwanza sikuona umuhimu wake kwa sababu ukitoa rushwa wale waliokuchagua wanakutazamaje?” alihoji Nagu.

Alikwenda mbali na kusema kuwa hata wananchi wake wa Hanang hawakufurahishwa na jinsi ambavyo alitendewa katika uchaguzi huo, na kwamba na wao wameamua kuchukua hatua ya kumuandikia barua Katibu Mkuu wa CCM.

Kauli hiyo ya Nagu imekuja ikiwa ni takribani mwezi mmoja tangu Sumaye atoe dukuduku lake, na kubainisha kuwa rushwa ya kimtandao, ndiyo iliyomwangusha wilayani Hanang.

Bila kumtaja Lowassa, huku akisisitiza kuwa hana uhasama naye, lakini kauli zake zilionekana wazi kumlenga Waziri Mkuu huyo wa zamani.

Sumaye ambaye mara baada ya kubwagwa na Dk. Nagu alikutana na wanahabari kuelezea mwenendo mzima wa uchaguzi huo na hatma ya CCM, alisema uchaguzi huo uligubikwa na matumizi makubwa ya rushwa, vitisho, uharamia wa kuhamisha wapigakura usiku na ukiukwaji mwingine mkubwa wa uchaguzi.

Alisema hajakata rufaa kupinga matokeo hayo wala kupeleka malalamiko katika chama chake kwa sababu yaliyokuwa yakitendeka yalikuwa yanafahamika.

Akifafanua kuhusu vitendo vya rushwa ndani ya CCM, Sumaye alisema kuwa nchi nyingi hasa zenye demokrasia changa kama Tanzania zimeingia katika vurugu na kuhatarisha amani na utulivu nyakati za uchaguzi.

---
Imeandikwa na Ratifa Baranyikwa, Dodoma, Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment