Sunday, November 11, 2012

Picture
picha: zenjydar.co.uk
KUMEKUWAPO na ongezeko kubwa la ajali za barabarani katika miaka ya karibuni kiasi cha kufanya abiria wanaotumia vyombo hivyo kukosa uhakika wa kufika waendako tofauti na miaka ya nyuma, ambapo usalama ulikuwa wa uhakika.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini kuwa ajali nyingi za vyombo vya usafiri hasa kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha Mbeya na Tanga hutokana na madereva wengi kuendesha wakiwa wamelewa.

Uchunguzi huo umebaini kuwa chupa ambazo hukaa kwenye ‘dashi bodi’ za magari mengi ya abiria zikionekana kuwa na maji, huwa ni pombe kali  ambazo madereva huzinywa wakati wakiendelea na kazi ya kuendesha magari wakisafirisha abiria.

Mbali na madereva hao wa magari ya mikoani, madereva wengi katika majiji hasa wa daladala wamekuwa 
wakiendesha  huku wamelewa ambapo hutembea na kinywaji hicho wakiwa wamekiweka kwenye chupa za maji safi ya kunywa ili kuwafanya abiria waamini kilichomo kuwa ni maji, lakini ukweli ni pombe.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga anaeleza kuwa kati ya mwaka 2005 hadi Juni 2012 ajali zilizotokea ni 11,163, vifo vikiwa 1,808 na majeruhi 9,155. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa ajali za pikipiki kuanzia mwaka 2007 hadi Juni 2012 ni 2,641,vifo 487 na majeruhi 2,706.

Mpinga alifafanua  kuwa ukilinganisha takwimu za ajali za barabarani kati ya mwaka 2010 na 2011,  ajali zilipungua kwa ajali 679 sawa na asilimia tatu, lakini vifo vimeongezeka kwa asilimia 11 sawa na watu 399 huku majeruhi pia wakiongezeka kwa asilimia 0.7. Alieleza kuwa ajali za pikipiki kwa mwaka 2011 zilikuwa 5,384 ikilinganishwa na ajali 4,363 zilizotokea mwaka 2010. Alisema kuwa hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 23 za ajali ambapo vifo vilikuwa 945 ikilinganishwa na vifo 683 vya mwaka 2010 ambapo majeruhi walikuwa 5,506 wakati mwaka 2010 kulikuwa na majeruhi 4,471.

Baadhi ya madereva wa vyombo vya usafirishaji wa abiria wa daladala wa  Dar na Morogoro waliozungumza na Mwananchi Jumapili, walikiri kuwapo kwa vitendo hivyo viovu vinavyohatarisha maisha ya abiria.

Mmoja wa madereva hao aliyeomba kutoandikwa jina gazetini, alisema kuwa mchezo huo umeanza siku nyingi akieleza kuwa na madereva wengi huweka konyagi kwenye chupa za maji na kunywa wakiwa kazini kwa kile wanachoeleza ili kupata stimu ya kufanya kazi.

"Ni kweli tunaweka konyagi huku,” alisema huku akishika chupa ya maji iliyokuwa kwenye dashi bodi na kuongeza: “Baadhi ya trafiki wametushtukia na kuna kipindi wanakagua. Unajua kazi ya kushinda unazunguka na gari   inachosha ndiyo sababu tunatafuta stimu."

Aliongeza: "Karibu madereva wengi tunafanya hivi. Unajua nyinyi mmezoea ofisini mnapigwa na kiyoyozi, sisi barabarani abiria wengine wehu, bila kulewa huwezi kukabiliana nao. Lakini pia hatuna muda wa kukaa baa kama nyinyi, ndiyo maana tunakunywa tukiwa kazini."

Baadhi ya madereva wa bodaboda jijini Dar es Salaam na Morogoro pia walikiri kuwapo kwa tatizo hilo wakieleza kuwa hutembea na pombe aina ya viroba na konyagi mifukoni ambazo huzinywa mara kwa mara.

Aidan Onesmo dereva wa bodaboda mkoani Morogoro alisema kuwa hufanya kazi hiyo kwa mashaka kutokana na kutosajiliwa, lakini pia kuhofia usalama wake kutokana na wezi wa pikipiki kuwa wengi. Anafafanua kuwa kutokana na hali hiyo hunywa pombe hiyo ya viroba ili kuondoa hofu anayokumbana nayo na kwamba hufanya hivyo kutegemea muda alioanza kazi, ambapo hutumia vingi kadiri anavyokaa muda mrefu zaidi kazini.

"Tunauawa kila siku, hii ni kazi ya hatari sana, bila kufanya hivi unaweza kumwogopa kila anayekuja kukukodi. Lakini ukinywa viroba, unaweza kwenda popote na mtu yeyote kwani unakuwa na stimu za kutosha," alisema Onesmo.

Kwa upande wao madereva wanaoegesha bodaboda zao maeneo ya Mabibo walikiri kunywa viroba wakiwa kazini wakieleza kuwa wanafanya hivyo ili kuondoa uchovu.

“Pamoja na kuondoa uchovu hatuna fedha za kunywa bia au kukaa baa kuagiza, hivyo tumeona kitu rahisi kisichohitaji muda mwingi wa kukaa kusubiri kiishe ni kiroba, tena kinapunguza gharama kwa kuwa ni rahisi,” alisema mmoja wa madereva hao akikataa kuandikwa jina.

Mmoja wa watumiaji wa usafiri wa bodaboda, Elizabeth Msuya wa Muheza mkoani Tanga alisema kuwa hukumbwa na hali ya wasiwasi kila awapo safarini kutokana na kupoteza wanafamilia wengi kwa ajali za barabarani. Alisema kwa mwaka mmoja wa 2010, alipoteza ndugu watatu ambao ni baba yake mdogo na kaka zake wawili kwa ajali hizo. Anasema kuwa baba yake mdogo alipata ajali alipokuwa safarini kuelekea Kijiji cha Kabuku mkoani humo  kwa kutumia usafiri wa gari dogo aina ya Hiace na kaka zake wawili waliokuwa wamepakizana kwenye pikipiki walifariki baada ya kugongana na lori uso kwa uso.

Naye Sufiani Hamisi wa Dar es Salaam alisema kuwa kutokana na kushuhudia ajali nyingi katika usafiri wa pikipiki, hawezi kutumia usafiri huo.

“Hata kuwe na usafiri mgumu kiasi gani, siwezi kupanda pikipiki, kutokana na kushuhudia ajali nyingi za vyombo hivyo vya usafiri chanzo kikiwa ni uendeshaji mbovu,” alisema.

Kwa upande wake Kamanda Mpinga, alithibitisha pia kuenea kwa tabia ya madereva  kubeba abiria huku wakiwa wamelewa pamoja na baadhi yao wakitembea na vilevi vyao. Alisema wameshapokea kesi za aina hiyo na baadhi ya watuhumiwa wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria licha ya kuwepo kwa changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kupimia kilevi mwilini.

"Kesi kama hizo zipo na vijana wangu wamekuwa makini sana licha ya kupata ugumu wa utekelezaji kutokana na ukosefu wa vifaa vya kupimia kilevi mwilini na kwa kuwa madereva wameshastukia hilo na kujilinda hivyo inakuwa ngumu kumtambua kwa kumnusa,"alisema Mpinga.

Aliongeza kuwa changamoto nyingine ni wananchi wenyewe, ambao wakati mwingine wanakuwa wagumu kutoa ushirikiano kwa Askari wa Usalama Barabarani pindi wanapomtilia shaka dereva kwa kuona wanacheleweshwa. Alisisitiza kuwa iwapo wananchi wangekuwa pamoja na askari hao kwa kutoa taarifa, kazi ya kukomesha tabia hiyo ya ajabu ingekuwa rahisi.

"Tunaipinga tabia hii kwa nguvu zetu zote na abiria yeyote atakayemtilia shaka dereva, asisite kutoa taarifa na tutamchukulia hatua kali kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwa wale waliobainika kufanya kitendo hicho kibaya," alimalizia Mpinga.

---
Imenukuliwa kutoka kwenye gazeti la MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment