Thursday, October 11, 2012

Habari imeandikwa na Kennedy Kisula, HabariLeo, Lindi -- HALMASHAURI ya Wilaya ya Lindi mkoani Lindi imewafukuza kazi watumishi wake wanne akiwamo Mhasibu Mwandamizi kwa makosa mbalimbali mojawapo likiwa ni kusindikiza lori lililosheheni zao la korosho zisizolipiwa ushuru katika msimu wa mwaka jana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, Hijob Shenkalwah aliyasema hayo jana wakati alipozungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha kufunga mwaka wa fedha 2011/12, na kueleza kuwa watumishi hao walikuwa na makosa ya utoro kazini, kusindikiza lori la korosho na kutoa vizuizi njiani.

Alisema Mhasibu Mwandamizi wa halmashauri hiyo, Joseph Songoro anatuhumiwa kutenda makosa ya kusindikiza gari lililobeba korosho ambazo hazikulipiwa ushuru wa mamlaka hiyo. Alisema kosa hilo lilifanyika Novemba 27, mwaka jana na kuvunja kizuizi kilichopo Kijiji cha Madangwa kwa kutumia nguvu.

Alisema kosa hilo kwa Sheria za Utumishi wa Umma, Kanuni ya 42, Songoro alikwenda kinyume cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003. Alifafanua zaidi, alisema Kanuni ya 42((1) jedwali la kwanza "A" inaeleza kuwa mtumishi akipatikana na hatia adhabu yake ni kufukuzwa kazi.

Mkurugenzi huyo alisema mtumishi mwingine ni Peter Kahisi ambaye ni Tabibu II katika Kituo cha Afya Rutamba alihusishwa na kosa la utoro kazini kuanzia Novemba 16 hadi Mei 17, mwaka huu.

Alisema mhusika alipewa notisi na hati ya mashitaka ili ajieleze, lakini hakupatikana kwani hakuwapo katika kituo chake cha kazi na Kamati ya Uchunguzi ilithibitisha kutokuwapo kwake kazini.

Alisema kwa kosa hilo alivunja kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003 Kanuni ya 57 jedwali la kwanza "A" ambayo inaelekeza kuwa mtumishi wa umma akikosekana kazini kwa muda wa siku tano mfululizo bila ya sababu au kutotoa taarifa kwa mwajiri wake, atafukuzwa kazi.

Alisema watumishi wengine ni Hamisi Lunda, Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Mnamba aliyekuwa mtoro kazini kuanzia Mei 28, mwaka jana hadi Mei 17, mwaka huu.

Mwingine alikumbwa na kadhia hiyo ni Othmani Mrope ambaye ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Shuka utoro kazini kuanzia Oktoba 15, 2011 hadi kufikia Mei 17, mwaka huu.0 comments:

Post a Comment