Wednesday, October 3, 2012

Mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba

HOJA ya adhabu kwa viongozi wanaotumia vibaya madaraka, ni miongoni mwa zilizotawala kwa Watanzania wengi wanaotoa maoni kwa ajili ya Katiba mpya, huku baadhi ya wanajeshi wakipendekeza kiongozi wa uraia anyongwe, mwanajeshi apigwe risasi hadharani.

Wanajeshi hao wametofautina na wananchi uraiani, ambao wengi wanapendekeza kiongozi anayefanya ubadhirifu, aondolewe mara moja, ashitakiwe kabla ya kustaafu au hata baada ya kustaafu na wengine wakapendekeza magereza maalumu ya viongozi.

Akitoa maoni mbele ya wajumbe wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Mabadiliko ya Katiba katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), 411KJ Ruhuwiko, askari Mwita Nyansango (26), alisema adhabu hizo zitarudisha uwajibikaji kwa viongozi.

Mbele ya viongozi wakuu wa kambi hiyo, ambao waliombwa waruhusu wapiganaji hao wawe huru wakati wa kujieleza, Nyansango alisema viongozi wa sasa hawafuati maadili, wanatumia vibaya rasilimali za wananchi kwa kuwa Katiba iliyopo, haijaweka wazi namna ya kuwawajibisha.

“Katiba ijayo iweke wazi, kuwa kiongozi anayepewa dhamana ya kuongoza jamii, ikiwa ni waziri kafanya ubadhirifu, napendekeza anyongwe ili iwe fundisho, akija mwingine ajue kuna kitanzi, kwa sisi wanajeshi, apigwe risasi.

“Tunasikia mambo ya Dowans na Richmond na tunachukia kusikia yanaendelea, halafu wahusika wanapewa nafasi ya kujitetea na wakifika mahakamani, wanapigwa faini,” alisema Nyansango ambaye ana elimu ya darasa la saba.

Nyansango pia alisema askari wa JWTZ, Polisi, Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), hawapaswi kuitwa wanajeshi kwa kuwa majeshi ya ulinzi ni ya nchi kavu, anga na majini.

Hoja hiyo ilifafanuliwa na Luteni Hassan Tagalile, ambaye ana Shahada ya kwanza, aliyetaka Katiba ijayo ifafanue kati ya JWTZ, Polisi, Magereza na JKT, ni chombo kipi ni jeshi la ulinzi na kipi chombo cha usalama.

Sajini Amedius Haule (51), ambaye ni Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Songea Mjini, alipendekeza askari wa ngazi za chini ya koplo, wawe na mwakilishi bungeni, kwa madai kuwa wao ndio wanaokutana na machungu ya Jeshi.

Koplo Abeli Mtanzamo (29), alipendekeza mawaziri wasitokane na wabunge, kwa madai kuwa akiwa waziri anafanya ubadhirifu akijua atajiuzulu uwaziri na kubaki na ubunge.

Koplo Elina Mwakitinga mwenye Diploma ya Ualimu, alipendekeza sheria za Jeshi zitambuliwe na Katiba na wanaotunga wajulikane hadhi zao kielimu na kuongeza kuwa ana wasiwasi sheria za Jeshi kwa sasa si shirikishi na zimerithiwa tangu ukoloni na kutengeneza watawala na watumwa jeshini.

Naye Koplo Shaban Mrope (33), alisema Tanzania ina madini mengi, lakini viongozi wameingia mikataba ya miaka mingi na kusababisha hata mtoto atakayemzaa, asifaidike.

Alisema nchi ina maliasili nyingi na ilipaswa kutoa elimu na afya bure na kama Serikali imeshindwa kufuta mikataba hiyo na kuweka ya muda mfupi, ipishe Jeshi kwa muda lifute mikataba hiyo.

Hoja hizo zilizotolewa jeshini, zilitolewa pia katika mikutano uraiani, ambako adhabu zilizopendekezwa zilikuwa tofauti. Kuhusu adhabu kwa viongozi wabadhirifu, mkazi wa kata ya Ruhuwiko, Songea Mjini, Anthony Leonard (26), alitaka Rais asiteue Jaji ili apate uhuru wa kutoa hukumu.

Alipendekeza kuwapo magereza ya viongozi na kuhoji; “kwa nini hakuna kiongozi aliye gerezani? Au wao hawaharibu?” Kijana huyo alisema kama rasimu ya Katiba mpya itakuja na kipengele ambacho taasisi ya urais inaruhusiwa kuteua Jaji, hatapiga kura na kama kutopiga kura ni kosa, yuko tayari kwenda jela.

Mkazi mwingine wa kata hiyo, Pascal Ndunguru (64), aliyependekeza mbunge asiwe waziri, alimhoji kiongozi wa wajumbe hao wa Tume, Profesa Mwesiga Baregu aeleze kwa nini amekuja kusikiliza wananchi bila kufuatana na mbunge wao.

“Profesa, wewe umefika hapa, yuko wapi mbunge wetu? Tunasikia ni waziri na hicho ndicho hatutaki kusikia, mbunge asiwe waziri atutumikie wananchi,” alisisitiza.

Simon Haule (80), mwenye elimu ya darasa la nne, alipendekeza Rais akitoka madarakani asipewe mshahara hadi kufa, bali alipwe pensheni kama mstaafu katika utumishi wa umma.

0 comments:

Post a Comment