Saturday, October 6, 2012

CHAGUZI ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimeendelea katika maeneo mbalimbali nchini ambapo sura mpya zimezidi kutikisa na kuwabwaga makada wa muda mrefu.

Tanga Mjini

Mbunge wa Tanga Mjini, Bw. Omari Nundu, ameanguka vibaya katika kinyang’anyiro cha kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), baada ya kupata kura 127 kati ya kura 1,183 zilizopigwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu.

Uchaguzi huo ulikuwa na mchuano mkali kati ya Bw. Nundu na aliyekuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Bw. Salim Kisauji aliyeibuka ushindi baada ya kupata kura 556.

Kushindwa vibaya kwa Bw. Nundu ambaye alikuwa Waziri wa Uchukuzi, kunamuweka njia panda katika medani ya siasa. Baadhi ya wana CCM mjini hapa walidai kushindwa kwa Bw. Nundu ni ishara mbaya kwake kuweza kutetea kiti chake cha ubunge kwa tiketi ya CCM kwani idadi ndogo ya kura alizopata ni ishara kuwa hana nafasi tena katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Akitangaza matokeo hayo jana alfajiri, Msimamizi wa uchaguzi huo Bw. Acheny Maulid, alimtangaza Bw. Kisauji kuwa mshindi wa nafasi ya ujumbe wa NEC. Alisema kura zilizopigwa zilikuwa 1,183 wakati nane ziliharibika na kura 1,175 zilikuwa halali. Katika uchaguzi huo Bi. Saumu Bendera alipata kura 458 na Bw. Salehe Masoud akipata 34.

Katika nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tanga, kiti hicho kilichukuliwa na Bw. Kassim Mbuguni aliyepata kura 662,  akifuatiwa na Bi. Mwanshamba Pashua (354) ambapo Bw. Samwel Kamote ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya mbalimbali nchini alipata kura 200 na Bw. Salim Mazrui akipata 98. Kura zilizopigwa zilikuwa 1,034 zilizoharibika 18, ambapo kura halali zilikuwa 1,016.

Akizungumza baada ya kuthibitishwa kuwa mjumbe wa NEC, Bw. Kisauji, aliahidi kuendeleza mshikamano ili kuongoza harakati za kukiimarisha chama hicho, “Nitaongeza kasi ya kuisimamia kikamilifu Serikali Wilaya ya Tanga ambapo siku za karibuni, kulikuwepo na udhaifu mkubwa uliochangia kuleta malalamiko dhidi ya Serikali,” alisema na kuwa, aliyekuwa mpinzani wake Bi. Bendera ataendelea kushirikiana nae kuhakisha wanasimamia wote utekelezaji wa ilani ya chama hicho na kuzikomboa kata tisa zilizoko upinzani kutoka CUF ili zirejeshwe CCM.

Hata hivyo, aliyekuwa Mwenyekiti wa muda katika uchaguzi huo Bw. Athuman Makalo, aliwataka wagombea wote waende mbele kuelezea mazingira ya uchaguzi huo.

Baadhi ya wagombea walioshindwa waliondoka ukumbini ambapo Bi. Mwanshamba Pashua, ambaye alishika nafasi ya pili katika nafasi ya Uenyekiti wa CCM Wilaya, ndiye aliyekwenda kuwashukuru wapiga kura.

Bunda

Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, Wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, wapo katika ushindani mkali kila mmoja akihaha kusaka kura kwa wajumbe.

Katika uchaguzi uliofanyika jana, mgombea wa nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha, Bw. John Kitang’osa, ambaye ni Katibu wa mbunge wa Bunda, Bw. Stephen Wassira, alibwagwa na kijana Bw. Mukwabe Sila.

Mgombea mwingine katika nafasi hiyo alikuwa Bw. Sarate Mimi ambaye ni mmoja kati ya Maofisa Wakaguzi wa Ndani katika Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Nafasi ya Katibu Uenezi Wilaya ilichukuliwa na Bw. Janes Sariro, ambaye aliwabwaga Bw. Kondoro Bega na Bw. Juma Sanga.

Bw. Christopher Sanya, Bw. Makongoro Nyerere na Bw. Enock Chambili, ambao wanagombea nafasi ya Uenyekiti Mkoa, waliomba kura kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo ambapo uchaguzi huo utafanyika Oktoba 13 mwaka huu.

Akiomba kura kwa wajumbe hao, Bw. Sanya alisema vigogo ndani ya CCM ndio wanaoendekeza makundi hivyo ni vyema wanachama waingize sura mpya ili kuleta umoja ndani ya chama hicho, “Wanaodai kumaliza makundi ndani ya CCM wanasema kwa mdomo tu, lakini haitoki moyoni kwa sababu wameshika madaraka hayo siku nyingi, dawa ya kumaliza makundi ni kuwachagua makada wasioegemea upande wowote,” alisema Bw. Sanya na kuongeza: “Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, utakuwa mgumu kwa chama chetu kama viongozi ambao watachaguliwa wataendeleza siasa za makundi.”

Naye Bw. Makongoro Nyerere, alidai mwaka 2007 aliipokea CCM iliyosambaratika mkoani humo iliyojaa siasa ya chuki na makundi ambapo kazi aliyoifanya ni kurejesha umoja katika chama hicho. Alisema viongozi wa kitaifa ndio wanaosambaza tofauti zao hadi kwenye matawi ya chama na kusambaratisha wanachama.

Bw. Chambili alidai yeye ni kiongozi asiyeogopa upinzani na yuko tayari kuhakikisha hakuna jimbo ambalo litachukuliwa na upinzani mkoani humo kama watamchagua katika nafasi hiyo.

Hata hivyo baadhi ya wajumbe na makada wa CCM, walidai wagombea wote wa nafasi, wamekiuka agizo la Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, “Hivi karibuni akiwa mjini Dodoma kwenye kikao cha NEC, baada ya kupitishwa majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali, Rais Kikwete aliwahadharisha wagombea wa nafasi zote kutowafuata wapiga kura ili kuomba huruma yao kabla ya siku ya uchaguzi,” walisema wajumbe hao.

Same
Mkuu wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Bw. Clement Kapufi, aliibuka na ushindi katika nafasi ya wajumbe watano ambao wataiwakilisha Wilaya hiyo katika Mkutano Mkuu Taifa.

Wengine walioshinda katika nafasi hiyo ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bw. Christopher Irira, Ummy Mkumbwa, Bi. Veronica Mmbaga na Zabihuna Irigo.

Katika uchaguzi huo, Mwenyekiti wa CCM wilayani humo Bw. Augustine Kessy, alitetea nafasi yake baada ya kupata kura 855 dhidi ya Bw. Yahya Mnzava (324) na Azza Nisaghurwe (153).

Bw. Ali Mmbaga alishinda katika nafasi ya ujumbe wa NEC wilayani humo baada ya kupata kura 832, wakati Bw. Joseph
Kateri (438), ambapo Bw. Joseph Mnzava, alipita bila kupingwa kwenye nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha.

Mwanga

Mwenyekiti wa CCM aliyemaliza muda wake Bw. Urban Masewa, alitetea nafasi hiyo baada ya kupata kura 527 ambapo mpinzani wake Bw. Suleiman Mruttu aliepata kura 252.

Wakili wa kujitegemea Bw. Joseph Tadayo, alishinda ujumbe wa NEC wilayani humo baada ya kuzoa kura 535 dhidi ya Bw. Kuria Msuya, (255) na Kanali mstaafu Saidi Msuya (18).

Bw. Suleiman Mfinanga, alimrithi Waziri Mkuu mstaafu, Bw. Cleopa Msuya katika nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha,
baada ya kupita bila kupingwa.

Rombo
Bw. Wilbard Ringia alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wilayani humo kwa kura 398 wakati Bw. Rogatus Matoli (300), ambapo Bw. Evod Mmmanda, alishinda ujumbe wa NEC wilayani humo kwa kura 380, Bw. Calisti Shirima (311) na Bw. Sabas Asenga aliepata kura 15.

---
Taarifa hii ni kwa mujibu wa Waandishi wa habari Raphael Okello, Heckton Chuwa na Benedict Kaguo wa gazeti la Majira

1 comments:

  1. VIJANA WANATAKIWA KUJITOKEZA KWA WINGI KATIKA CHAMA CHA MAPINDUZI ,MUDA UMEFIKA WAKATI NI HUU WADAU CHAMA NI CHETU YA NINI KULUMBANA WANEC SHIRIKIANENI NA WABUNGE WENU KULETA MAENDELEO KATIKA MAJIMBO HUSIKA SIO KUCHUNGULIANA NANI KAINGIA NANI KATOKA MTAA UPI NAWE UZAME HAPOHAPO HATUFIKI MTATUMIA MUDA MWINGI KUTAFAKARI BADALA YA KUSONGA MBELE ,CHAIRMAN UVCCM MKINGA

    ReplyDelete