Wednesday, October 3, 2012

Habari na Magreth Chaba, BUKOBA via ChamaMagreth.blogspot.com --- Zimesalia siku 3 za kuuzika rasmi mwili Kadinali wa kwanza Afrika na Askofu wa kwanza Mwafrika, Mwadhama Laurean Rugambwa ambaye alizikwa kwa muda katika Kanisa la Kashozi mwaka 1997, hatimaye atazikwa rasmi katika kanisa kuu jimbo Katoliki la Bukoba, baada ya ukarabati wake kukamilika.

Askofu msaidizi wa jimbo Katoliki la Bukoba Methodius Kilaini alisema kuwa maamuzi ya marehemu Rugambwa kuzikwa Kashozi yalitokana na kanisa hilo alilochagua kuzikwa kuwa katika ukarabati tangu mwaka 1996.

Askofu Kilaini alisema kuwa mazishi hayo rasmi yatafanyika Oktoba 6 mwaka huu, siku ambayo pia itakuwa ni kumbukumbu ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Kadinali Rugambwa ambaye alizaliwa mwaka 1912, “Masalia  ya Kardinali Rugambwa yatahamishwa rasmi siku hiyo kutoka kanisa Katoliki la Kashozi, tutasherehekea miaka 100 ya kuzaliwa kwake, lakini pia siku hiyo Kanisa Katoliki jimbo la Bukoba litatabalukiwa” alisema.

Alisema kitendo hicho ni kumbukumbu  nzuri kwa Watanzania na Waafrika kwa ujumla kutokana na kuwa Kadinali wa kwanza Afrika na Askofu wa kwanza Mwafrika,  hivyo  wanategemea kupata wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi, na kwamba baada ya mazishi hayo kanisa hilolitaanza kutumika

Alisema kuwa baada ya shughuli hizo, Kanisa Katoliki jimbo la Bukoba linataendelea kutumika kwa ibada za kawaida, ili  kuwaondolea waamini wao adha ya kusalia katika ukumbi, “Tunaendelea kuhamasisha waamini wetu wachangie fedha kwa ajili ya kumalizia sehemu ya ujenzi iliyobaki, lakini pia wachangie sherehe hizo ili ziweze kufanyika kwa ufanisi” alisema Askofu Kilaini.

Akizungumzia historia ya Kadinali Rugambwa alisema kuwa alipewa Upadre mwaka 1943,  mwaka 1952 akapewa Uaskofu, mwaka 1960 akawa Kadinali na mwaka 1969 akawa Askofu Mkuu Dar-es-Salaam  hadi alipostaafu mwaka 1992.

Akigusia kidogo aliyoyafanya Kadinali Rugambwa ambayo baadhi yake yanawafanya watu waweke  kumkumbuka, Askofu Kilaini alisema kuwa alianzisha Kanisa kuu jimbo la Bukoba, alileta Seminari Kuu ya Ntungamo na alijenga shule ya Sekondari Rugambwa.

Mengine ni ujenzi wa hospitali ya Mugana, kuanzisha vikoba kwenye Parokia, kuanzisha Seminari ndogo ya Visiga na kuanzisha Seminari kuu ya Segerea iliyoko Dar-es-Salaam.

0 comments:

Post a Comment