Tuesday, October 30, 2012

Maafisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wametoboa siri hatua ya Naibu Waziri wa wizara hiyo, Philipo Mulugo, kukosea kutaja Zimbabwe badala ya Zanzibar kama kisiwa kilichounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakizungumza na NIPASHE jana, walisema pamoja na kwamba aliteleza kutaja Zimbabwe akimaanisha Zanzibar, kimsingi suala hilo linakuzwa na baadhi ya mahasimu wake wa ndani na nje wa kisiasa.

Walisema mahasimu wake hao ni wale ambao kwa namna moja au nyingine, wameathirika kutokana na misimamo yake anayoitoa hususan katika suala la kuzifunga shule na kuwatimua watendaji wanaobainika kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Mmoja wa maafisa hao ambaye aliambatana na Naibu Waziri huyo nchini Afrika Kusini, Enock Barnabas, alisema kimsingi makosa yaliyofanywa na Mulugo ni ya kibinadamu tu ambayo yanaweza yakafanywa na mtu yeyote.

Hata hivyo, alisema wameshangazwa kuona suala hilo linavyokuzwa na baadhi ya watu.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ufundi, David Kazuva, alisema ufafanuzi uliotolewa na Naibu Waziri kuhusu suala hilo, umeeleweka kwa jamii na wanaoendelea kulijadili wana lao jambo.

Maafisa hao walimtaka Mulugo kutokatishwa tamaa na watu wanaompiga vita na badala yake aendelee kutekeleza majukumu yake kwa sababu baadhi ya watu hawaangalii mafanikio ya mtu bali huangalia pale anapofanya makosa ndipo wapate cha kusema.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi ambao wamechangia hoja zao kwenye mitandao ya kijamii, walisema viongozi wengi wanaosafiri nje na ndani ya nchi, wamekuwa wakifanya makosa madogo kama hayo wanapowasilisha taarifa mbalimbali za serikali.

“Mti wenye matunda ndiyo upigwao mawe, tunamfahamu Mheshimiwa Mulugo kwa utendaji wake kazi na ndiyo maana watu wanataka kumkatisha tamaa kwa maslahi yao binafsi,” alisema Brown John.


---
Imenukuliwa kutoka kwenye gazeti la NIPASHE

0 comments:

Post a Comment