Sunday, September 2, 2012

Ayoub Mangi -  MAELEZO-Dar es Salaam -- Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeongeza mbele tarehe za kumaliza kazi ya Sensa ya Watu na Makazi hadi Jumamosi ya tarehe 8 Septemba mwaka huu ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi aliyebaki anahesabiwa.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Sensa kutoka NBS Hajjat Amina Mrisho Said wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu masuala mbalimbali yaliyohusu kazi nzima ya Kuhesabu Watu na Makazi inayoendelea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Alisema ni vema wananchi ambao hawajafikiwa na Makarani wa Sensa watoe taarifa katika Ofisi za Serikali za Mitaa au Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa ajili ya kuhesabiwa.

Hajjat Amina alisema taarifa zinazotakiwa ni pamoja na taarifa za wanakaya waliolala katika kaya yao usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti mwaka huu.

Alitoa wito kwa wale ambao hawajaandikishwa hadi hivi sasa kuwa wanatakiwa watume taarifa kwa namba 2122724, 0754583415, 2129622 , 0713335429, 0713574622 na 0713312699 .

Hajjat aliongeza kuwa katika taarifa watakazopeleka ni vema wakaeleza mitaa au kijiji au kitongoji gani walipo ili iwe rahisi kwa NBS kutambua karani mhusika na kumwelekeza afanye kazi hiyo.

Aidha, Kamishina huyo alisema malipo ya makarani yalishafanyika kwa awamu ya kwanza kulingana na mkataba na wanatarajia kuwalipa awamu ya pili mara baada ya kazi zao kuhakikiwa na wasimamizi wao. Aliongeza kuwa kwa wasimamizi watalipwa baada ya kazi zao kukamilika na kuhakikiwa na waratibu katika ngazi za wilaya.

Kuhusu malipo ya Wenyeviti wa Vijiji , Vitongoji na Mitaa, alisema fedha zao walishapelekwa siku nyingi na maelekezo ya namna ya kuzigawa yalipelekwa kwa Waratibu wa Sensa wa Mikoa na Wilaya ambao walipaswa kuwa wameshalipa ili kuepusha manung’uniko.

Katika hatua nyingine, Kamishna wa Sensa huyo amewaonya kuwa Karani yeyote atakayechakachua taarifa na ikathibitika hivyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria. Ameongeza kuwa NBS inafuatilia taarifa kutoka Dodoma eneo la Kisasa kuwa kuna Karani amekwenda kwenye kaya lakini alikuwa haulizi maswali.

Wakati huo huo, Hajjat alisema kuwa wale viongozi wengi waliokuwa wakiwahamasisha wenzao wasihesabiwe, wamehesababiwa kwa hiari baada ya kutoa ushirikiano wa kutosha ikiwemo kuacha taarifa muhimu zilizohitajiwa ikiwemo zile zilihitajika katika madodoso. Kwa wale ambao hawakuwakuta, waliweka alama maalum ili wawarudie mara ya pili. 


0 comments:

Post a Comment