Saturday, September 15, 2012

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema ameishauri Serikali kudhibiti warsha za mara kwa mara na zitakazokubalika ziwe na mitihani ambayo matokeo yake watapewa mabosi wa watahiniwa.

Akizungumza katika semina ya waandishi wa habari kuhusu namna ya kuripoti masuala ya rushwa kutokana na ripoti za CAG, Utouh alisema tayari mfumo huo umeanza katika Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali.

Kwa mujibu wa Utouh, katika kila warsha hasa zinazozidi siku tano, washiriki wa warsha hizo watapaswa kufanya mtihani na matokeo ya mtihani kuhusu mada zilizojadiliwa, yatapelekwa kwa mabosi wa washiriki.

Alifafanua kuwa, mabosi hao watatakiwa kutumia matokeo hayo katika kupandisha vyeo watumishi walioshiriki katika semina hizo au vinginevyo.

Alisema katika ofisi yake ya NAOT wameanza kutumia mfumo huo ambapo warsha zote zinazozidi siku tano, washiriki hulazimika kupewa mitihani na matokeo ya mtihani huo huwasilishwa kwake.

“Sisi tumeanza mfumo huu ambao unasaidia kutambua value for money, (thamani halisi) warsha yoyote inayozidi siku tano, washiriki hupewa mtihani na matokeo yao yaliyowasilishwa kwangu huyatumia kuwapromoti au kuwaadhibu,” alisema.

Alikuwa akijibu swali la mmoja wa washiriki wa warsha iliyoandaliwa na ofisi yake ambaye alitaka kujua hatua zilizochukuliwa na NAOT katika kudhibiti warsha za mara kwa mara za taasisi za Serikali zisizo na tija.

Pamoja na hayo Utouh alibainisha wazi kuwa ofisi yake imekuwa ikifanyakazi kwa uhuru wa kutosha hasa ikilinganishwa na ofisi nyingine zinazofanyakazi kama hiyo ya ukaguzi duniani, “Na hii ni kutokana na ukweli wa Sheria iliyotumika kuanzisha NAOT ambayo inabainisha wazi kuwa ni kosa kama mtu au taasisi isipotoa ushirikiano wa kutupatia taarifa tunazozohitaji katika ukaguzi wetu,” alisema.

Lakini pia kutokana na uwezo na taaluma za wafanyakazi wa ofisi hiyo ya CAG, wamekuwa wakiaminika ndani na nje ya nchi ambapo hivi karibuni walifanya ukaguzi wa hesabu za Umoja wa Mataifa (UN) na Shirika la Maendeleo la UN (UNDP) ambalo hesabu zake ni kubwa zaidi ya bajeti ya Tanzania.

Akizungumzia suala la magari ya gharama kubwa yanayotumiwa na Serikali, Utouh alisema moja ya kazi ya ofisi ni pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu namna ya kupunguza na kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali.

Alisema NAOT imekuwa ikiishauri Serikali kwa muda mrefu katika manunuzi yake ya magari ya Serikali kuzingatia ununuzi wa magari yenye gharama nafuu jambo ambalo kwa sasa limeanza kuzaa matunda, “Tulishawahi kukagua ununuzi wa magari na kubaini kuwa magari mengi ya Serikali yanayonunuliwa ni ya gharama kubwa na yanatumia mafuta mengi, tukaishauri Serikali kuwa magari ya aina hii si ya lazima,” alisema na kuongeza, “Tuliwahoji, je kiongozi akiwa jijini Dar es Salaam anahitaji VX kutoka Mikocheni hadi katikati ya jiji? Suala la warsha za mara kwa mara limekuwa likipigiwa kelele hadi kufikia Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuingilia kati na kupiga marufuku warsha na semina zisizo na tija.

via HabariLeo


0 comments:

Post a Comment