Tuesday, August 28, 2012

Wachezaji wa Yanga wakiteremka kutoka kwenye ndege baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere wakitokea Kigali, Rwanda jana. Picha na Doris Maliyaga
Sosthenes Nyoni
MABINGWA wa Kombe la Kagame, Yanga wamerejea nyumbani wakitokea ziarani Kigali, Rwanda bila ya beki wake mpya Mbuyu Twite anayetarajia kuwasili leo na kujiunga na kambi ya timu hiyo.

Ziara ya Yanga nchini Rwanda ilitokana na mwaliko ilioupata kutoka kwa Rais Paul Kagame ambaye ni mdhamini mkuu wa michuano ya Kombe la Kagame.

Mbuyu aliyekuwa gumzo la jiji baada ya kujisajili na timu hasimu, Simba na baadaye Yanga, aliomba muda zaidi akamilishe masuala mbalimbali ya kifamilia kabla ya kuja Tanzania kujiunga na timu hiyo.

Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet alipoulizwa sababu za kutoambatana na Twite katika msafara wake, kwa kusema ni kutokana na ombi la beki huyo walimwacha ili akamilishe mambo yake ya kifamilia.

"Ni sahihi kabisa umeniuliza swali ambalo najua mashabiki pia watapenda kufahamu, ni kwamba Twite  atakuja kesho [leo] sasa wasiwe na wasiwasi, aliomba akamilishe mambo yake," alisema Mbelgiji huyo.

Juzi klabu ya Simba kupitia kwa Makamu wake, Geofrey Nyange 'Kaburu' alidai kuwa watamkamata mara atakapoteremka na kikosi cha Yanga jana kwani tayari wameshamchukulia (Twite) RB ya polisi.

Hatua hiyo imetokana na kile kilichoelezwa kuwa alichukua fedha za Simba Dola 30,000 wakati akisaini kuichezea timu hiyo kabla ya Yanga 'kupindua mtumbwi' na sasa anatakiwa kulipa Dola 39,500 kama fidia kwa kuvunja na gharama za usumbufu.

Kukosekana kwake katika kikosi kilichowasili, kulizusha hisia hizo kukwepa pingu za Simba, ambao hata hivyo Mwananchi iliangaza uwanjani hapo bila kumuona kiongozi yeyote wa mabingwa hao wa aliyefika kumkabili Twite endapo angefika.

Ukiacha hayo, katika ziara hiyo,Yanga ilicheza mechi mbili za kirafiki  ikiwa ni dhidi ya Rayon Sport na kushinda mabao 2-0 kisha kuifunga Polisi Rwanda mabao 2-1.

Msafara wa Yanga uliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere majira ya saa tisa alasiri na kulakiwa na mshabiki wachache ambao baadhi yao walionekana kuvalia fulana zenye jina la Mbuyu Twite.

Akizungumza uwanjani hapo, Saintfiet alisema kuwa ziara yao ilikuwa ya mafanikio hasa katika maandalizi kwa msimu ujao wa ligi.

"Kimsingi ziara yetu imekuwa na mafanikio...Shirikisho la Soka Rwanda, Ferwafa, na mpaka katika mechi zetu za kujipima nguvu tulizocheza, walitupa ushirikiano wa hali ya juu,"alisema Saintfiet na kuongeza:

"Kilichobaki tunatambua kwamba  nyuma yetu kuna mashabiki wetu ambao  hakuna kitu kingine wanachohitaji zaidi ya kuurudisha ubingwa mikononi mwetu na hilo ndilo deni tulilonalo."

Wakati huo huo, Saintfiet alisema kikosi chake kesho kitajitupa kwenye dimba la Uwanja wa Taifa kuikabili Mafunzo ya Zanzibar ikiwa katika muendelezo wa mechi zake ya kujipima nguvu kabla ya msimu mpya wa ligi kuanza.

Alisema kuwa programu ya timu yake inayohusu mechi za kirafiki itakamilika kwa pambano jingine dhidi ya AFC Leopard itakayopigwa kwenye uwanja huo Jumamosi ijayo.

0 comments:

Post a Comment