Friday, August 31, 2012



Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara cha kampuni ya Precision Air, Patrick Ndekana(kushoto)akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mkataba na Vodacom Tanzania ambapo wateja wataweza kulipia tiketi za usafiri kupitia huduma ya M-Pesa,kulia ni Mkuu wa kitengo cha huduma za fedha wa Vodacom Tanzania Bw. Innocent Ephraim.
*******
Kampuni ya usafiri wa anga ya Precision air hii leo imeingia kwenye mkataba na Vodacom Tanzania ambapo wateja wataweza kulipia tiketi za usafiri kupitia huduma ya M-Pesa.

Ili kufanya malipo mteja atatakiwa kupiga namba *150*00# na kuchagua malipo ya bili kupitia orodha ya M-pesa na kuingiza namba ya biashara ya Precision Air ambayo ni 333777  ikifuatiwa na namba ya malipo na kiasi cha fedha itakayolipwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ushirikiano huo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara cha kampuni ya Precision Air, Patrick Ndekana, amesema kuwa njia hiyo ni ya haraka, rahisi na itaokoa muda kwa wateja.

“Tunafurahi kuingia katika ushirikiano huu na Vodacom Tanzania, Tunawahimiza wateja wetu kutumia huduma hii ili kuokoa muda na kufanya malipo yao katika njia ambayo ni rahisi na ya haraka,” alisema Ndekana.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Huduma na Kifedha cha Vodacom Tanzania, Innocent Ephraim, alibainisha kuwa ushirikiano huo utatoa njia badala katika malipo ya tiketi, na kusisitiza kuwa huduma ya M- pesa ni salama, haraka na niya uhakika, kwa kuwa imeleta mapinduzi katika huduma mbalimbali za kifedha tangu kuanzishwa kwake miaka mimne iliyopita.

“Tunaamini kuwa tutatoa huduma bora kwa wateja wetu. Tunajivunia ushirikiano huu na tunatarajia utakuwa na mafanikio makubwa katika kukidhi mahitaji ya huduma kwa wateja wetu,” alisema Ephraim.

Huduma ya M-Pesa ya Vodacom Tanzania ina mawakala zaidi ya elfu 20,000 nchini kote, na ni pekee ambayo inaongoza, kwa usalama na ubora katika kukidhi mahitaji ya huduma za kifedha kwa Watatanzania walio wengi.

Kampuni ya Precision Air inatoa huduma zake katika mikoa mbalimbali ya Tanzania, na kufika katika maeneo mengi ya nchi kwa siku.

Sasa kampuni hiyo ina ndege tano zenye uwezo wa kubeba abiria sabini aina ya ATR 72-500, na ATR 42 yenye uwezo wa kubeba abiria arobaini na nane na ndege nyingine tatu aina ya Boeng 737. Na sasa iko katika mpango wa kuongeza ndege nyingine aina ya E- jets na ATR.
Mkuu wa kitengo cha huduma za fedha wa Vodacom Tanzania Bw. Innocent Ephraim,akionesha bango lenye maelekezo muhimu ya kufuatwa ambayo yatawafanya wateja wapate huduma ya kulipia tiketi za usafiri kupitia huduma ya M-Pesa kwa urahisi zaidi,kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara cha Precision Air, Patrick Ndekana.
Baadhi ya wafanyakazi wa Precision Air wakifatilia kiumakini mkutano wa waandishi wa habari kuhusiana na mkataba wa Vodacom Tanzania na kampuni yao ambapo wateja wa Precision Air wataweza kulipia tiketi za usafiri kupitia huduma ya M-Pesa.
Waandishi wa habari wakiwa kazini wakati wa Precision Air na Vodacom Tanzania walipokuwa wakitangaza mkataba kuhusiana na wateja wa Precision Air kuweza kulipia tiketi za usafiri kupitia huduma ya M-Pesa.

0 comments:

Post a Comment