Wednesday, July 4, 2012

Afya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dkt. Steven Ulimboka imeendelea kuimarika baada ya kupata matibabu nchini Afrika  Kusini na sasa figo zake zimeanza kufanya kazi.

Dkt. Ulimboka alipelekwa nchini huko mwishoni mwa wiki baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kiasi cha kusababisha figo zake kushindwa kufanya kazi.

Katibu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dkt. Rodrick Kabangila alisema Dar es Salaam jana kwamba, hali ya Dkt. Ulimboka imeimarika na kuwaomba Watanzania wamuombee apone haraka.“Taarifa tulizozipata kutoka Afrika Kusini zinasema kwamba,  hali ya Dkt. Ulimboka imezidi kuimarika tofauti na alivyokwenda, figo zimeanza kufanya kazi ingawa kwa polepole na amefanyiwa vipimo vingine,” alisema Dkt. Kabangila na kuongeza:

“Pia ameanza kuzungumza, anawatambua watu vizuri na zaidi amewaomba Watanzania wamuombee apone haraka.”

Awali, chanzo kimoja cha habari kilidokeza kwamba  hali ya Dkt. Ulimboka imeimarika kutokana na kupatiwa huduma za matibabu kwa haraka kwa kufanyiwa vipimo vingine. Pia Dkt. Ulimboka anafanyiwa usafishaji damu na figo (Dalysis), mara kwa mara. Kabla ya kuondoka nchini, Dkt. Ulimboka alifanyiwa usafishaji huo mara mbili.

Madaktari walisema usafishaji huo ulilenga  kupunguza kiwango cha sumu iliyoonekana  kwenye damu, ambayo haikutambulika mara moja kama ilitengenezwa ndani ya mwili au vinginevyo kwa kuwa hakuna kipimo cha kubaini tatizo hilo nchini.

0 comments:

Post a Comment