Saturday, June 30, 2012


Mgomo wa madaktari ulianza Juni 23 na madaktari wanazidi kujiunga na mgomo huo baada ya kutekwa na kupigwa kwa Dkt. Steven Ulimboka

Jana, Ijumaa, JJeshi la polisi nchini Tanzania lilisema kuwa litaanza kuwakamata madaktari wanaoshiriki katika mgomo wa madaktari nchini humo kwa sababu wanakiuka amri ya mahakama.

Akizungumza na waandishi wa habari Ijumaa jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Paul Chagonja alisema jeshi la polisi lina kila sababu ya kuwakamata madaktari wanaogoma. Alisema kama madaktari hawakukubaliana na pingamizi ya serikali walikuwa na haki ya kukata rufaa sio kuendelea na mgomo.

Katika habari nyingine madaktari wanasema Dkt. Steven Ulimboka ambaye alitekwa na kupigwa na watu wasiojulikana mapema wiki hii anahitaji kufanyiwa vipimo zaidi nje ya nchi.

Wakati huo huo, madaktari bingwa wa serikali za umma Ijumaa walitangaza kujiunga na mgomo kupinga kupigwa kwa Dkt. Ulimboka. Jeshi la polisi limeunda tume watu watano kufanya uchunguzi wa mkasa wa Dkt. Ulimboka lakini tume hiyo imepingwa na wengi ikiwa ni pamoja na madaktari wenyewe.

Dinah Chahali
VOA - Swahili

0 comments:

Post a Comment