Saturday, June 30, 2012

Kuna taarifa kuwa siku ya kesho, Jumapili, Julai Mosi, 2012, kila kitu kilichokuwa katika hospitali ya Taasisi ya Moyo (Tanzania Heart Institute - THI) kitapigwa mnada.

Wapo watu waliopelekwa huko kuthaminisha vitu vyote inasemekekana vitu vyote lazima vipigwe mnada.
Mwezi Aprili 2012, Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kupitia amri ya mahakama, iliifunga taasisi hiyo na kuwahamishia wagonjwa wote kwenye hospitali nyingine kwa kile kilichoripotiwa ni Taasisi hiyo kushindwa kulipa Shilingi bilioni 7 za pango.

Matangazo yaliyokuwepo kwenye majengo ya hospitali hiyo yalitoa taarifa ya kufungwa kwa hospitali hiyo na kudai kwamba tayari amepatikana mwekezaji mwingine anayetaka kutumia majengo hayo yaliyo barabara ya Tunisia karibu na klabu maarufu ya viongozi ‘Leaders Club’ wilayani Kinondoni.

Tangazo hilo lililokuwa na kichwa cha habari "taarifa kwa umma" lilisema NSSF inatoa taarifa kwa wananchi wote kuwa, kwa mujibu wa amri ya Mahakama Kuu (kitengo cha Ardhi) iliyotolewa Septemba 11 mwaka jana katika shauri na 158/2007 kati ya NSSF na Taasisi ya moyo Tanzania, “Hospitali hii imefungwa kwa amri ya Mahakama. Jengo ni mali ya NSSF na limepata mwekezaji mwingine” “NSSF itatwaa jengo lake lililojulikana kama "Hosteli ya Tazara" ambapo kwa sasa limepangishwa na THI Julai 25 mwaka huu hivyo wagonjwa wote na familia zao wanashauriwa kufanya mpango mbadala ya hospitali ya kuhama au kuhamisha wagonjwa wao kabla ya tarehe hiyo kufika.” ilinukuliwa sehemu ya taarifa hiyo.

Akizungumza na gazeti la HABARILEO Jumapili kuhusu suala hilo, Meneja Uhusiano wa NSSF, Eunice Chiume, alisema ni kweli taasisi hiyo imefungwa na vifaa vyake kushikiliwa na madalali wa Mahakama kwa sababu mmiliki wake alishindwa kulipa kodi ya pango ya zaidi ya Sh. bilioni 7.

Akizungumzia hatua walizopata kuchukua kabla ya kuamua kuifunga ili walipwe, Chiume alisema walikuwa wakimkumbusha mpangaji kuhusu kulipa au kupisha jengo hilo bila mafanikio na badala yake, miaka mitatu baada ya kukabidhiwa jengo hilo na kushindwa kulipa, alikimbilia mahakamani kuzuia kuondolewa.

Taarifa za NSSF zinasema Dk. Massau alikabidhiwa jengo hilo mwaka 2004 na kuachiwa mwaka mmoja wa kuendesha shughuli zake bure, ili ajipange sawa sawa lakini aliendelea kulitumia bila kulipa hadi alipofungiwa.

Chiume alisema zimejitokeza hospitali kadhaa zinazotaka kupanga, ikiwamo ya Apollo ya India na kwamba wako katika mchakato wa kuangalia kwa undani wampangishe nani ili kuepuka yaliyotokea yasijirudie.

Dkt. Massau alikiri kudaiwa kiasi hicho cha pango na kusema sababu za kutolipa zilikuwa wazi kwa shirika hilo.

“Ni kweli wananidai, lakini wanajua kesi ilikuwa mahakamani na tulipaswa kurudi huko Aprili 24, ili kujua kinachoendelea, lakini wamekuja kuvamia usiku wa Aprili 10, na kupiga watu na kubeba wagonjwa kuwapeleka kusikojulikana, tumelalamika mpaka kwa Jaji Mkuu na tutafika mahakamani siku hiyo ya kesi, tukiwa na malalamiko yetu juu ya kukiukwa kwa sheria,” alisema Dkt. Masau.

Alikanusha kupangishwa mwaka 2004 na kudai kuwa alikabidhiwa jengo hilo la ghorofa mbili Mei 2005 likiwa na kasoro nyingi zilizofanya washindwe kuendesha shughuli za upasuaji wa moyo na hivyo kuendesha huduma za matibabu mengine ya moyo tofauti na makubaliano na wafadhili. 
Picture
Dkt. Masau
Mwaka 2008, Dkt. Masau aligoma kuhama katika jengo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa mkutano wa VC uliopo ndani ya Jengo la Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) muda mfupi baada ya kumalizika kwa semina ya madaktari wa moyo mwaka huo, alisema yeye hawezi kuhama katika jengo hilo kwa sababu NSSF imeshindwa kutimiza makubaliano yao wakati walipompangisha na kuongeza, “Kwanza siwezi kuhama katika jengo hilo kwasababu kuna wagonjwa 15 wamelazwa ambapo kati yao wagonjwa 5 wanategemea kufanyiwa upasuaji wa moyo wakati wowote, pili vitu ambavyo viko ndani ya jengo hilo ni zaidi ya bilioni, makubaliano yetu ilikuwa ni kutengeneza jengo hilo ili liwe na hadhi ya hospitali ya moyo kitu ambacho walishindwa kuyatimiza,” alisema Dkt. Masau.

Alisema moja ya makubaliano yao ni kwamba NSSF wamtengenezee jengo liwe na hadhi ya Hospitali ya Moyo.

Alisema baada ya makubaliano hayo NSSF walimpelekea taarifa kuwa kazi hiyo imeshamalizika hivyo anachotakiwa kufanya ni kukubali kusaini mkataba wa kulipangisha jengo hilo.

“Nilikubali kusaini mkataba wa kama mpangaji baada ya NSSF kunihakikishia kuwa wamenitengenezea jengo hilo kama nilivyowaeleza, lakini baada ya kusaini mkataba na kuingia ndani ya jengo nikagundua kuwa kuna baadhi ya maeneo hayajatengenezwa kama nilivyoyahitaji,”alisema Masau na kuongeza:

“Baada ya kubaini mapungufu hayo tulikubaliana niendelee kulitumia jengo hilo wakati marekebisho hayo yanafanyika, lakini hayo hayakufanyika badala yake nilishangaa kuona taarifa ya kuitwa mahakamani kwa kesi ya madai miezi miwili baada ya mkataba huyo,”alisema.

Alifafanua kuwa baada ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa mahakamani miezi miwili baadaye hukumu ilitolewa na mahakama ikaamuru aondolewe katika jengo hilo na kwama baada ya amri hiyo alimfuata Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambapo Waziri aliwataka wayamalize nje ya mahakama chini ya Wizara ya Kazi Ajira na Maendeleo ya Vijana.

Hata hivyo, kufuatia taarifa za ndani ya NSSF zilizonaswa na gezeti MWANANCHI, Serikali ilishawahi kutoa tamko kuwa haiwezi kingilia zaidi mgogoro huo na kuwataka wamalize mgogoro huo kwa mujibu wa maamuzi ya mahakama.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo za siri pia ilibaini kuwa Julai 5, Waziri wa Kazi Ajiri na Maendeleo ya Vijana wa wakati huo, Profesa Juma Kapuya alimuandikia Dkt. Masau barua iliyosema kuwa endapo atashindwa kulipa sehemu ya deni hilo kama walivyokubaliana katika kikao cha Julai Mosi mwaka huu NSSF itaendelea na uamuzi wake wa kumtoa ndani ya jengo hilo.

“Tulikubaliana kuwa endapo taasisi yako itashindwa kulipa sehemu ya deni hilo kama inavyopendekezwa basi NSSF itaendelea na uamuzi wake wa kuitoa hiyo THI kwenye jengo hilo kama iliyoamuriwa na mahakama bila kutoa notisi nyingine,”ilisema sehemu ya barua hiyo ya Waziri Kapuya.

Hata hivyo, nakala ya barua ilipelekwa kwa Waziri Mkuu,Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na NSSF.

---
picha via Charaz.blogspot.com

Source: WAVUTI

0 comments:

Post a Comment