Friday, June 22, 2012



Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Ayoub Mangi
JUMUIYA ya Madaktari imetangaza rasmi kuanza kwa mgomo usio na kikomo kuanzia kesho, huku ikidai Serikali imekataa kutekeleza madai yao yote yaliyowasilishwa katika kamati ya majadiliano iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.Wakati madaktari hao wakitangaza kurejea rasmi katika mgomo huo uliositishwa miezi mitatu iliyopita, Pinda aliliambia Bunge jana wakati akijibu Maswali ya Papo kwa Papo, kuwa mgomo huo ni batili na haukubaliki.

Saa chache baada ya Pinda kutoa onyo hilo lililorushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni na redio kutoka Dodoma, madaktari hao wakiwa jijini Dares Salaam walitangaza mgomo huo wenye lengo la kushinikiza Serikali kutekeleza madai yao.

Mgomo huo ulitangazwa kwa waandishi wa habari na Dk Stephen Ulimboka, muda mfupi baada ya kukamilika kwa mkutano wa ndani wa madaktari, uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Utamaduni la Watu wa Urusi.

Dk Ulimboka alisema mgomo huo usio na kikomo utawahusu madaktari wa kada zote nchini, na unatarajiwa kuanza kesho, baada ya wiki mbili walizotoa kwa Serikali kumalizika bila ya makubaliano yoyote.

“Madaktari kwa ujumla wao wamekubaliana kuwa watarejea katika mgomo usio na kikomo, hii ni kutokana na kugundua kuwa hakuna dhamira ya dhati ya Serikali, kumaliza mgogoro kati yetu na Serikali, uliodumu kwa muda mrefu sasa,” alisema Dk Ulimboka na kuongeza,

“Serikali imetupilia mbali madai yote yaliyofikishwa katika meza ya majadiliano baina ya wawakilishi wa Serikali na madaktari na taarifa iliyotolewa bungeni na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi na pia majibu ya Waziri Mkuu leo, yamepotosha kila kilichomo katika taarifa tuliyonayo sisi.”

Alifafanua kwamba Serikali imetupilia mbali madai yote ambayo kabla ya kukubali kurudi katika meza ya majadiliano yalionekana kuelekea kupata mwafaka.

Dk Ulimboka alisema kuwa kauli iliyotolewa na Pinda bungeni, kwamba walikubaliana, si ya kweli na hata posho zilizotajwa kwenye taarifa za kamati hiyo ni za dharura kabla ya kuanza kwa vikao vya majadiliano.

Alisema msimamo wao ni kuanzisha mgomo usio na kikomo na hakuna njia ya mkato ya kuuzuia, njia pekee ni Serikali kurudi katika meza ya majadiliano.

Kuhusu ushauri uliotolewa na Pinda kuwataka waende mahakamani, Dk Ulimboka alisema jumuiya yao haiko tayari kwenda na kwamba itaendelea na utaratibu wake wa kushinikiza madai hayo kwa njia ya mgomo.

“Sisi hatuendi mahakamani na hakuna njia yoyote ya kuuzima mgomo zaidi ya kurudi kwenye meza ya majadiliano yenye lengo la kufikia mwafaka wa yale tunayotaka kukubaliana," alisisitiza.

Alisema katika madai yao ya msingi waliyotoa serikalini, hadi sasa limetekelezwa moja tu, huku wakishangazwa na Serikali kuongeza posho ya uchunguzi wa maiti kutoka Sh10,000 za awali hadi Sh100,000 kwa madai kuwa posho hiyo haikuwa miongoni mwa madai yao.

“Sisi katika madai yetu hatukuliweka dai hili la posho ya uchunguzi wa maiti, kwa sababu hilo siyo dai letu la msingi. Kazi ya uchunguzi wa maiti siyo ya kila wakati, hufanywa tu pale watu wanapokuwa na mashaka na kifo cha mtu husika, lakini pia haifanywi na madaktari wote,” alisema Dk Ulimboka.

Madai ya madaktari

Katibu wa Jumuiya hiyo, Dk Edwin Chitega alitaja madai yaliyowasilishwa katika kamati hiyo kuwa ni hali bora ya mazingira ya utoaji afya nchini, ongezeko la mishahara, posho za kufanya kazi katika mazingira magumu, posho za kufanya kazi katika mazingira hatarishi na posho za kuitwa kazini.

Akizungumzia dai la hali bora ya mazingira ya kazi, alisema hadi sasa hakuna kilichotekelezwa huku hali ya utoaji huduma kwa wagonjwa ikizidi kuwa mbaya.

“Tunaweza kusema tangu tukubali kuingia kwenye meza ya majadiliano hali imezidi kuwa mbaya. Katika hospitali kubwa kama Muhimbili inakosa vitendea kazi, dawa, wagonjwa kulazwa chini huku rufaa za wagonjwa kwenda nje ikiongezeka,” alisema Dk Chitega na kuongeza:

“Tunachotaka sisi ni huduma za afya ziboreshwe ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora za afya na kupunguza rufaa za kwenda nje kutibiwa.”

Dk Chitega alitoa mfano wa gharama zilizotumika kwa mwaka wa fedha wa 2010/11, kuwa ni Sh7 bilioni, ilhali fedha zilizotumika kwa kipindi cha mwaka huu kwa ajili ya uendeshaji hospitali kubwa sita za hapa nchini kuwa Sh5 bilioni.

“Tulipendekeza pia mchakato wa rufaa uboreshwe kwa kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje kwa kuboresha huduma za ndani, Serikali ilianzisha Taasisi ya Mifupa (MOI), ikapeleka madaktari kwenda kusoma India, wamekuja kufanya kazi wamekosa vifaa wameondoka. Sisi lengo letu ni kuona fedha za nchi zinatumika kuwasaidia Watanzania,” alisema Chitega.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Dk Godbles Charles alisema taarifa zilizotolewa bungeni na Pinda na Dk Mwinyi zimepotoshwa na zina lengo la kuwarejesha kwenye mgomo.

Pinda awaonya

Mjini Dodoma, Pinda alitoa taarifa jana kwamba suala hilo liko Mahakama ya Kazi na kuonya kwamba mgomo huo ni batili, wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.

Mbowe alitaka kujua hatua zilizofikiwa na Serikali katika kutatua mgogoro wa madaktari na walimu nchini, na sababu za kutotekelezwa makubaliano yaliyofikiwa katika majadiliano.

Akijibu swali hilo, Pinda alisema Serikali iliunda tume kushughulikia mgogoro wa madaktari ambapo kulikuwa na madai 10 yaliyojadiliwa na kati ya hayo, madai matano yalifikiwa mwafaka na madai mengine matano bado yanaleta mvutano.

“Ni kweli tumekuwa na mgogoro na madaktari lakini tumekuwa tukizungumza nao kwa kipindi chote cha tatizo hili, ili kupata mwafaka na kwa kama mwezi mmoja tume iliyoundwa ilimaliza kazi na kuwasilisha taarifa serikalini kwa ajili ya kufikia maamuzi,” alisema Pinda.
 
Pia alisema Dk Mwinyi alijitahidi kuonana na madaktari lakini haikuwezekana, ndipo akamshauri awaandikie barua ambayo madaktari walimjibu kuwa, hawaoni haja ya kuendelea na mazungumzo, kwani wamekuwa wakifanya kwa karibu miezi mitatu bila mafanikio.

Waziri mkuu alisema, baada ya Serikali kufikia hatua hiyo, ikaona ni vyema sasa irudi kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa kuwa hawakuafikiana.

Alisema kwenda CMA si mara ya kwanza, kwani awali walikwenda lakini Serikali ikashauri ni kwa nini wasijadiliane nje na kufikia mwafaka, na baadaye kurudi CMA ili kuandikisha makubaliano waliyofikia.

“Hivyo tumerudi tena CMA kutoa taarifa na sasa suala hili limepelekwa mahakamani, lakini kama Jumamosi wakianza mgomo ni kinyume cha sheria… mimi nina wasihi sana, bado ipo nafasi ya kufikia mwafaka,” alisema Pinda.

Alisema mambo matano ambayo wamefikia mwafaka ni kuongeza malipo ya uchunguzi wa mwili wa marehemu kwa madakari ambapo wasaidizi sasa watalipwa Sh50,000 na madaktari Sh100,000.

Pia alisema Serikali ilikubali kuwaondoa mawaziri na watendaji wengine wa wizara hiyo, imeongeza malipo ya kuitwa kwa dharura na mengine kadhaa.

Waziri Mkuu alisema mambo ambayo hawajafikia mwafaka ni pamoja na ongezeko la mishahara ya madaktari, posho ya usafiri na nyumba na  posho za kufanya kazi katika mazingira magumu.

Mgogoro wa walimu

Kuhusu walimu, Pinda alisema hatua iliyofikiwa hivi sasa ni nzuri kwani tayari chombo cha majadiliano ambacho kilikuwa bado, sasa kimeundwa.

Alisema tayari Katibu Mkuu, Utumishi, amempatia taarifa za kukamilika kwa chombo hicho ambacho sasa kitawezesha kufikiwa makubaliano ya msingi na hivyo kutatua matatizo ya walimu.

Waziri Mkuu, alitoa angalizo kutokana na ujumbe wa simu unaosambazwa, ambao hata hivyo hakuufafanua, na kuomba kusiharakishwe kufikia huko kwani baada ya muda mfupi mwafaka wa madai ya walimu utapatikana.

Ujumbe huo ambao umesambazwa katika mitandao ya kijamii, unasomeka: “Hebu tizama tofauti hii ya kutisha ya viwango vya mishahara kwa watumishi wa umma wa TZ (Tanzania); (Ajira mpya cheti) mwalimu Sh244,400, Afya Sh472,000, Kilimo/Mifugo Sh959,400, Sheria Sh630,000.
Diploma: Mwalimu Sh325,700,  Afya Sh682,000, Kilimo/Mifugo Sh1,133,600, Sheria Sh871,500.

“Degree (shahada) Mwalimu Sh469,200, Afya Sh802,200, Kilimo/Mifugo Sh1,354,000,  Sheria Sh1,166,000. Je upo tayari kuvumilia kunyanyaswa hivyo katika utumishi wa umma wa taifa moja lenye soko la bidhaa lililo na mfumuko wa bei wa kutisha? Ungana na CWT kudai nyongeza ya mishahara 100%, Teaching allowance (posho ya kufundisha), hardship allowance (posho ya mazingira magumu). Wape sms hii walimu 20 tu! Mshikamano daima.”

0 comments:

Post a Comment