Friday, June 22, 2012


Msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael, 'Lulu'.
Mawakili wa upande wa Jamhuri katika kesi ya mauaji ya Steven Kanumba (28), inayomkabili msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, wamewasilisha katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam vielelezo vya kuthibitisha kwamba mshtakiwa huyo ana umri wa miaka 18.
Vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani, ni pamoja na CD iliyorekodi mahojiano kati ya mtangazaji wa Clouds TV, Zamaradi Mketema, maelezo ya kuomba hati ya kusafiria na leseni ya udereva.

Pia umewasilisha mahakamani hapo maelezo ya polisi pamoja na maombi ya hati ya kusafiria ambapo mshtakiwa ameeleza kwamba ana umri zaidi ya miaka 18.

Kesi hiyo itasikilizwa Juni 25, mwaka huu, mbele ya Jaji Dk. Faiz Twaib mahakamani hapo.
Juni 13, mwaka huu, mawakili wa utetezi, Peter Kiabatala, Fuljensi Massawe na Kennedy Fungamtama, waliwasilisha vielelezo kwa njia ya maandishi kupitia kiapo.
Katika ushahidi uliowasilishwa, baba mzazi wa Lulu, Michael Kimemeta, ameapa kwamba, binti yake hadi anatuhumiwa kufanya mauaji, umri wake ni miaka 17.

Kalugila, ambaye ni mama mzazi wa Lulu naye pia anadai kuwa alijifungua mtoto huyo miaka 17 iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam.
Upande wa Jamhuri unaoongozwa na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimario, utajibu ushahidi huo Juni 20, na maombi hayo yatasikilizwa Juni 25, mwaka huu.
Lulu anakabiliwa na shtaka la mauaji dhidi ya msanii mwenzake, Kanumba Aprili 7, mwaka huu, katika eneo la Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.
                                            CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment