Tuesday, June 19, 2012

Na Makongoro Oging'
KATIKA hali isiyokua ya kawaida waalikwa katika harusi ya wachumba wawili walipigwa na butwaa baada ya ndoa kutofungwa kanisani kufuatia bi harusi kuwa na ujauzito.
Kasheshe hiyo ilitokea hivi karibuni katika Kanisa la Pentecoste la Abundant Blessings Centre (ABC) lililopo Tabata Relini, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam katika ndoa iliyotarajiwa kufungwa kati ya wachumba waliojulikana kwa jina mojamoja la Eli na Naomi.

Taarifa zilizopatikana kwa baadhi ya waumini na ndugu zilidai kwamba Jumapili moja jamaa wa pande zote mbili wa bwana na bi harusi watarajiwa walikuwa kanisani huku wakiimba kwa furaha na vigelegele wakiwasubiri maharusi wawasili.
Hata hivyo, muda ulizidi kwenda bila watarajiwa hao kuonekana kanisani katika muda uliopangwa, hali iliyomfanya mchungaji wa kanisa hilo, Flaston Ndabila kuendelea na zoezi la kufungisha ndoa nyingine kwani siku hiyo ilipangwa zifungwe mbili.

Katika ndoa hiyo ambayo hata hivyo haikufungwa mwanaume ni mwenyeji wa Mkoa wa Mbeya na mwanamke ametokea mkoani Shinyanga.
Chanzo kilidai kwamba ilipofika saa 7.00 mchana mchungaji akawatangazia waumini, ndugu na jamaa wa pande zote kwamba ndoa ya Eli na Naomi haitafungwa kwa kuwa mwanamke alikuwa ni mjamzito.
Habari zaidi zilieleza kwamba mara baada ya kutangazwa hivyo baadhi ya wanandugu wa pande zote mbili walichanganyikiwa na wengine kudondoka chini na kupoteza fahamu kwani hawakutarajia kama hali hiyo ingejitokeza.

Vyanzo viliendelea kusema kwamba mama wa bwana harusi mtarajiwa alichanganyikiwa zaidi na kuishiwa nguvu jambo lililosababisha apate msaada wa kushikiliwa na watu.
Mwandishi wa habari hii alimtafuta Mchungaji Ndabila ili kupata ukweli wa habari hii ambapo alikiri ndoa hiyo kutofungwa kwa sababu mwanamke alikua mjamzito.
“Kulingana na taratibu zetu za kikanisa kama bi harusi mtarajiwa ana mimba hatuwezi kufungisha ndoa,” alisema mchungaji huyo.

0 comments:

Post a Comment