Sunday, May 13, 2012

Mwali bado kafichwa kwa sababu mwenye dau kubwa bado hajajulikana, japokuwa ni kati ya wababe wawili wa Manchester - Manchester City na Manchester United.
Man.united ushindi 2009
Bingwa 2009 Man.United
Timu hizi mbili zina pointi 86, lakini City wana mabao mengi manane kuliko United.
Kwa kuzingatia hayo, mechi muhimu zaidi Jumapili hii ni ile inayozikutanisha Manchester City na Queen Park Rangers (QPR), mchezo unaofanyika Etihad, nyumbani kwa City mbele ya washabiki wake.
Mechi nyingine inayotia wadau matumbo joto ni ile ya Manchester United na Sunderland, United safari hii wakichezea ugenini.
Ili City watwae ubingwa wanatakiwa kuwa na matokeo kama ya United au mazuri zaidi. Kwa kifupi ni kwamba, City wakishinda kuna uwezekano mkubwa wa kutangazwa wafalme wa soka wa England.
Ferguson
Mazowea ya Ferguson kila mwaka
Ni katika hali hiyo Kocha Mkuu wa Manchester United, Sir Alex Ferguson anasema wao wanaombea litokee jambo la 'kijinga' dhidi ya jirani zao (Manchester City) ili wanyakue tonge mdomoni mwao. Kwamba wao United watatekeleza wajibu wao kujitahidi kushinda mechi yao, lakini kulipata kombe itategemea nyumba ya jirani.
Lakini ikumbukwe kwamba vijana hao wa Roberto Mancini katika msimu wote wamepoteza pointi mbili tu katika uwanja wao huo wa Etihad, yaani wameshinda mechi zote isipokuwa mbili tu walizotoka sare.
Ndiyo maana washabiki wao wengi wana matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa walioupata mara ya mwisho mwaka 1968. Wanachotegemea dhidi ya QPR ni ushindi tu.
QPR wananolewa na kocha wa zamani wa City, Mark Hughes aliyetupiwa virago Desemba 2009 baada ya kushinda mechi mbili tu kati ya 11 City walizocheza mfululizo. Kocha huyo pia ameichezea United na Ferguson anamtegemea 'amsaidie kuiangamiza City'. Kwa ujumla timu mbili hizi za Manchester zinatarajiwa kuibuka na ushindi kwenye mechi zao hizi za mwisho.
Ligi ya Mabingwa Ulaya
Moja ya mambo yanayotafutwa kwenye mbio za Ligi Kuu ya Uingereza ni nafasi za timu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa minajili ya Uingereza wakati huu, panaweza kuwapo nafasi moja au mbili, wakati timu zinazowania ni Arsenal wenye pointi 67,
Tottenham waliojikusantia pointi 66 na Newcastle waliovuna pointi 65.
Mechi muhimu katika kuamua hili ni kati ya Everton na Newcastle; Tottenham Hotspur dhidi ya Fulham na West Brom wanaoikaribisha Arsenal.
Hali ilivyo ni kwamba hatima ya Arsenal imo mikononi mwao wenyewe, kwa maana kwamba wanachotakiwa ni kushinda tu ili kufuzu moja kwa moja, bila kusubiri matokeo ya mechi nyingine. Ushindi utawahakikishia kubaki nafasi ya tatu wanayoshikilia
Hata hivyo, ikiwa Arsenal watatoa sare dhidi ya Baggies, wanaweza kuvukwa na kutupwa nafasi ya nne ikiwa Tottenham watawafunga Fulham.
Maana yake ni kwamba Washika Bunduki hao wa London hawatakuwa na chaguo zaidi ya kuingia kwenye mechi za mchujo ili kufuzu, huku Spurs wakisonga moja kwa moja kwenye mashindano hayo makubwa ya Ulaya.
Ikiwa Arsenal watachezea kichapo nyumbani kwa West Brom, ni dhahiri pia watakuwa wamejiweka pabaya, kwa sababu wataweza kupitwa na Spurs watakaohitaji sare tu
ikiwa Arsenal itafungwa mabao mawili au zaidi. Arsenal pia watapitwa na Newcastle inayonolewa na Alan Pardew, ikiwa watawafunga Everton.
Vinginevyo ni kwamba Tottenham wakishinda mechi yake tu itakuwa imejihakikishia kupata nafasi ya nne na sare pia inaweza kuitosheleza ikiwa Newcastle hawatawafunga Everton.
Kwa upande mwingine, ili Newcastle waweze kuingia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lazima wawafunge Everton na kuomba ama Arsenal au Tottenham wasishinde mechi zao. Ikiwa hizo tatu zitatokea, basi Newcastle itamaliza ligi ikiwa katika nafasi ya tatu.
Hata hivyo, ikiwa Chelsea itatwaa Kombe la Mabingwa Ulaya kwenye fainali dhidi ya Bayern Munich mjini Munich Mei 19 mambo yatabadilika Uingereza, kwa sababu timu itakayoshika nafasi ya nne kwenye EPL mwaka huu haitakuwa na nafasi kwenye ligi hiyo tena.
Badala yake, timu hiyo itaingia kwenye Ligi ya Europa pamoja na watakaomaliza ligi wakiwa nafasi ya tano, kwani timu inayotwaa kombe hilo inashiriki msimu unaofuata kulitetea.
Katika mazingira haya, Arsenal watatakiwa kutumia vyema nguvu na fursa kuwamaliza West Brom, kwani kwao msimu ni kama umeshaisha tu, hawana kikubwa cha kupata wala kupoteza.
Spurs wanaelekea pia kwamba watawafunga Fulham, na maana ya haya ni kwamba kuna kila dalili za Newcastle kuachiwa simanzi bila kupenda.
Pengine Bayern watalitwaa kombe la Ligi ya Mabingwa, na kwa kufanya hivyo mazingira ya Ligi kuu ya England na ushiriki wa msimu ujao kimataifa kutoathiriwa.

0 comments:

Post a Comment