Tuesday, May 15, 2012

VUGUVUGU la kisiasa katika jimbo la Iringa mjini, limezidi kupanda joto baada ya Mbunge wa jimbo hilo, kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mchungaji Peter Msigwa kudai kuwa ametishiwa kuuawa kwa maneno na Diwani wa kata ya Nduli, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamis Chonanga.

Hatua ya mbunge kudaiwa kutishiwa kuuawa imemfanya mbunge huyo kutoa taarifa katika kituo cha polisi cha Iringa mjini.

Hali hiyo inatokana na vurugu za kisiasa zilizotokea juzi katika mkutano wa hadhara wa Chadema, uliofanyikia kata ya Nduli, ambao ulisababisha baadhi ya vijana kumvamia Mchungaji Msigwa wakitaka kumcharanga mapanga na kusababisha majeraha kwa vijana watatu wa Chadema.

Katika mkutano huo, Mchungaji Msigwa alinusurika kucharangwa mapanga baada ya kundi la vijana wanaoaminika kutokea CCM  kumvamia kwa madai ya kukerwa na kundi la watu zaidi ya 90 akiwemo Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji, Ayubu Mwenda kuamua kujiunga na chama hicho. Waliojeruhiwa huku mmoja wao akilazwa katika hospitali ya Mkoa wa Iringa, Wodi namba tano ni Oscar Sanga, Perter Mselu na Saleh Komba.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa, Mchungaji Msigwa alisema akiwa katika viwanja vya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, alipata vitisho kutoka kwa diwani Chonanga ambaye alidai kuwa, alisema lazima amuue kutokana na kumfuata fuata.

 “Asubuhi nikiwa pale Manispaa, alikuja Chonanga akaniambia lazima aniue mimi na diwani wa Chadema, kata ya Mivinjeni, Frank Nyalusi ili tukome kumfuata fuata…hii inatokana na vurugu zilizotokea juzi kwenye kata yake, baada ya kuchukizwa na kundi la wananchi wake, kuhamia Chadema jambo lililowafanya vijana wake kujeruhi kwa mapanga,” alisema Mchungaji Msigwa.

Msigwa alisema baada ya kutishiwa huko, aliamua kutoa taarifa polisi , ili jeshi hilo lifanye kazi yake, kwa madai kuwa kutishiwa kuuawa ni kosa la jinai na kwamba baada ya taarifa hiyo jeshi hilo lilimtia mbaroni kiongozi huyo.

Hata hivyo alisema ikiwa Polisi hawatachukua hatua dhidi ya jambo hilo, Chadema itahakikisha wanasimamia haki ili nguvu ya umma ichukue mkondo wake.

“Hatutaendelea kushuhudia vijana wetu wakiumizwa na sisi tukistishiwa maisha, polisi kama hawatachukua hatua, basi nguvu ya umma iitachukua mkondo wake,” alisema Mchungaji Msigwa.

Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Mivinjeni, Nyalusi alisema baada ya taarifa yao polisi, walishuhudia diwani huyo kukamatwa  jambo lililowafanya waamini sheria inachukua mkondo wake.

“Diwani alikamatwa baada ya taarifa na tunatarajia kumpeleka mahakamani ili sheria ichukue mkondio wake,” alisema Nyalusi.

Wakati Msigwa akisema kuwa, ametoa taarifa jeshi la polisi kwa kutishiwa kuuawa, Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Evarist Mangala alisema hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na  mbunge huyo kuhusu kutishiwa kuuawa.

Naye ofisa mnajibu wa jeshi la Polisi Mkoani Iringa, Bundala Msiba alisema kuwa kilichopo polisi ni taarifa vurugu za kisiasa zilizoripotiwa wakati wa mkutano uliofanyika nduli.

 “Suala la kukamatwa kwa diwani sio kweli, lakini kilichoripotiwa ni makosa madogo mdogo ya kisiasa tu, kuhusu vurugu za nduli,” alisema Bundara.

0 comments:

Post a Comment