Wednesday, May 16, 2012

NDANI ya Tasnia ya Filamu Bongo kuna kitu na kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni kila msanii kwa nafasi yake kumuomba Mungu amuepushe na kila la shari, Risasi Mchanganyiko lina ripoti kamili.
Hilo limebainika kufuatia matukio ya kusikitisha ambayo yamekuwa yakiwakumba wasanii katika siku za hivi karibuni na kuacha maswali mengi kwa wadau.
Wasanii ambao wanaingia katika listi ya kufikwa na mazito achilia mbali Steven Kanumba aliyefariki dunia, ni pamoja na Juma Kilowoko ‘Sajuki’, Irene Uwoya, Kajala Masanja, Elizabeth Michael ‘Lulu’, Skyner Ally ‘Skaina’, Wema Sepetu, Blandina Chagula ‘Johari’ na Aunt Ezekiel.
KIFO CHA KANUMBA
Tasnia ya filamu Aprili 7, mwaka huu ilimpoteza Kanumba ambaye alifariki dunia wakati bado mchango wake unahitajika katika jamii. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi-Amina.
UGONJWA WA SAJUKI
Huku kifo cha Kanumba kikiendelea kuwatesa mashabiki wake, msanii mwingine, Sajuki naye anasumbuliwa na uvimbe kwenye ini, mazingira yaliyosababisha apelekwe nchini India kwa matibabu.
Mungu amjaalie apone haraka na arudi katika majukumu yake ya kuiburudisha na kuielimisha jamii.
NDOA YA UWOYA
Ndoa ya staa huyu aliyeolewa na msakata kabumbu wa Timu ya Rayon Sports FC ya Rwanda, Hamad Ndikumana ‘Kataut’ imekumbwa na dhoruba kufuatia kuibuka mazingira ya kusalitiana yaliyosababisha kila mmoja achukue hamsini zake.
Hata hivyo, taarifa zilizo chini ya kapeti zinadai Uwoya amekuwa akifanya jitihada kuhakikisha anairudisha ndoa yake.
LULU, KAJALA KUTUPWA SEGEREA
Wasanii hawa wana wakati mgumu na kwa sasa wapo katika Gereza la Segerea wakikabiliwa na kesi tofauti.
Lulu anakabiliwa na kesi ya kuhusishwa katika kifo cha Kanumba huku Kajala akikabiliwa na kesi ya kutakatisha fedha haramu.
NDOA YA SKAINA
Mwanzoni mwa mwaka huu, Skaina alifunga ndoa na Omari Saad lakini ndoa hiyo ilidumu kwa takribani siku nne, wakamwagana.
Skaina aligoma kueleza chanzo cha kuvunjika kwa ndoa hiyo ingawa baadaye ilibainika mumewe alimkuta na ujauzito ambao haumhusu.
WEMA KUNUSURIKA KUUAWA
Miezi michache iliyopita, upepo mbaya uliendelea kuitafuna tasnia ya filamu ambapo Wema alikutwa na msala wa kutaka kugongwa na gari la mwanamke aliyemtuhumu kumuibia mume wake.
AJALI YA JOHARI
Januari 25 mwaka huu, Johari aliingia kwenye listi ya waliokumbwa na majanga baada ya kupata ajali mbaya maeneo ya Ubungo ambapo gari lake aina Toyota Opa liliharibika vibaya ila hakujeruhiwa.
AUNT KUVAMIWA
Naye Aunt juzikati alivamiwa na majambazi kwenye pub yake iliyopo Mwananyamala, Komakoma, Dar.
Kwa bahati nzuri yeye alikuwa ametoka ila wateja wake walikombwa fedha pamoja na vitu vya thamani.
MSANII WA UBAKAJI
Tukio ‘karenti’ ni la msanii aliyecheza filamu ya Kijiji cha Tambua Haki na marehemu Kanumba, Soud Muhogo kutupwa Segerea akituhumiwa kumbaka msanii chikupiki wa filamu (jina kapuni).
JB ANANENA
Akizungumza kwa masikitiko kuhusiana na matukio hayo, Mwenyekiti wa Bongo Movie, Jacob Steven ‘JB’ alisema ni wakati wa wasanii kumuomba Mungu kwa kuwa majaribu yamewaandama sana mwaka huu.
“Tunawaomba Watanzania watuombee ili Mungu atuwezeshe kuyashinda haya majanga yanayotuandama kwani sala zao ndizo zitakazotunasua na kutufanya tuendelee na kazi hii ya sanaa kwa ufanisi na ubora wa hali ya juu.
“Pia sisi kama wasanii kila mmoja kwa imani yake apige goti na kumuomba Mungu ili atuepushe na matatizo haya. Ni wakati wetu wa kufunga na kuomba katika hili.”
Picha zilizotumika ukurasa wa nyuma ni za baadhi ya wasanii wa filamu Bongo, kati yao wamefikwa na majanga mbalimbali na wengine wameumizwa na matatizo yanayoitesa tasnia yao.

0 comments:

Post a Comment