Friday, May 4, 2012

Baadhi ya wananchi wametoa maoni tofauti kuhusiana na matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha sita wa mwaka huu.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma , Paul Loisulie, amezitaka shule nchini kujifunza kwa Marian ya Bagamoyo, mkoani Pwani na Feza ya Dare s Salaam na kusema  shule hizo zimekuwa zikiongoza kila mwaka katika matokeo ya mitihani hivyo kuna cha kujifunza kutoka kwao ili ziweze kufanya vizuri.
“Mwaka huu angalau matokeo yanaonyesha shule za serikali zinaweza kufanya vizuri , kati ya shule bora 10, sita ni za serikali  hili ni jambo zuri,” alisema.

Mwalimu katika shule ya vipaji maalumu ya  Sekondari ya kidato cha tano na sita ya Kwiro wilayani Ulanga mkoa wa Morogoro, Mariki Kindamba, alisema kuna haja kwa Serikali kulingalia Baraza hilo la Mitihani upya kwani limekuwa likipendelea baadhi ya shule zenye majina kila mwaka na wanafunzi wake kuwawekea alama za juu hata kama hawana uwezo.

Kindamba ambaye kwa sasa anasoma shahada ya pili katika Chuo Kikuu Huria, alisema hali hiyo imekuwa ikipelekea wanafunzi wa shule hizo zisiokuwa na majina kupunguziwa maksi zao kwakuwa hawana sehemu ya kuwapeleka.
Naye  Omary Selemani, mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Kislamu alisema kuna tatizo lingine kwa upande wa walimu wakuu na walimu wa kawaida katika baadhi ya shule hizo ndio maana wanafunzi wanashindwa kufanya vizuri.
Amir Wesai, mkazi wa Soweto jijini Mbeya, alisema kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu kunaonyesha kuwa Serikali imeanza kurekebisha kasoro zilizokuwepo.
Mkazi wa Forest jijini Mbeya, Joyce Mwandalima, alisema matokeo hayo yanaonekana ni mazuri kutokana na uchache wa shule za kidato cha sita na kudai kuwa juhudi zaidi zinahitaika.
Mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rabson Emmanuel, alisema ufaulu wa mwaka huu ni mzuri, lakini cha kushangaza shule za binafsi zinazidi kufanya zaidi kuliko za serikali.
Mwanafunzi mwingine wa chuo hicho, Miriamu Makeba, aliwapongeza wasichana kwa kuongoza katika mtihani huo na kuwataka walioko mashuleni kuiga mfano huo.

Imeandikwa na Emamanuel Lengwa, Mbeya,  Sharon Sauwa, Ashton Balaigwa, Morogoro na Leonce Kimbandu, Dar.

CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment