Saturday, May 26, 2012

WATU sita wamefariki dunia na wengine wawili wamejeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kuanguka na kusababisha watu wengine wawili kujeruhiwa vibaya katika eneo la Sigino wilayani Babati mkoani Manyara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa amesema ajali hiyo imetokea jana saa 2 asubuhi wakati gari la mizigo lililokuwa na tela lenye namba za usajili T 536 AGH na tela lenye namba za usajili T 575 BHJ mali ya Josephat Mkalama wa mjini Babati, likitokea Iringa kuja mkoani hapa, lilipoacha njia na kuanguka baada ya breki zake kushindwa kufanya kazi.
Kamanda Mpwapwa amewataja waliokufa kuwa ni pamoja na dereva wa gari hilo, Paulo Charles (38) mkazi wa Mafinga mkoani Iringa, utingo, mama mmoja aliyetajwa kwa jina la Juliana Joseph (35) mkazi wa Sinai wilayani Babati pamoja na mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili, ambao walikuwa wakitokea Singida. Marehemu wengine wanne majina yao hayakuweza kufahamika mara moja.
Kamanda Mpwapwa amewataja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Anjelina Basiri (65) mkazi wa Sigino, Babati na kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Lazaro (15) mkazi wa Dongobesh wilayani Mbulu, ambao walikuwa kando ya barabara nje ya nyumba wanayoishi walipofuatwa na kukumbwa na ajali.
Majeruhi hao wamekimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Babati (Mrara) ambako wanapatiwa matibabu, huku hali zao zikiwa ni mbaya, na kwamba Anjelina anapumua kwa msaada wa mashine maalumu, na kijana Lazaro akiwa ameumia vibaya mguu wake wa kushoto akiwa hajitambui. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya.
Ajali hiyo imetokea wakati juzi mkoani Mwanza, watu watano walikufa hapo hapo na wengine watano kujeruhiwa vibaya baada ya gari la mizigo walilokuwa wakisafiria kutoka mkoani Shinyanga kwenda Mwanza kupinduka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Hawa Charles (30), Ngereja Nzeso (25), Tabu Mwage (22) ambao ni wakazi wa Malampaka mkoani Shinyanga na wengine wawili hawakutambuliwa.
WALIOKUFA AJALI YA MBUNGE WAFIKIA WANNE
Katika tukio jingine, idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali ya gari iliyomhusisha Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA) imeongezeka na kufika watu wanne baada ya mmoja kufariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma alisema hadi sasa waliotajwa kufa ni pamoja na mama mzazi wa mbunge huyo, Catherine Roman Selasini (80), mama mkwe wake, Agatha Jerome Mahoo (85) na wanawake wawili, mmoja ikidaiwa ni shangazi yake ambao majina yao hayajajulikana.
Majeruhi kwenye ajali hiyo ni pamoja na mke wa Selasini, Digna Kavishe (43) ambaye amepata majeraha sehemu za kichwa na hali yake si nzuri, pamoja na mbunge huyo ambaye amepata majeraha kwenye bega pamoja na mkono wa kulia.
Ajali hiyo ilitokea juzi saa 1.00 jioni katika barabara kuu ya Moshi, Arusha eneo la Chuo cha Ufundi Bomang’ombe wilayani Hai, baada ya gari lenye namba za usaji T 441 BRT aina ya Toyota Land Cruiser lilikuwa likiendeshwa na Selasini kupinduka.
chanzo cha habari: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=36313

0 comments:

Post a Comment