Monday, April 30, 2012



WALIMU  6,000 wa shule za sekondari na msingi katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam wamesema   hawatashiriki sherehe za wafanyakazi  Mei Mosi zitakazoadhimishwa kesho katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi jana Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT), Manispaa ya Ilala, Emmanuel Kihako alisema wamekataa kushiriki kwa kuwa mwajiri wao amewabagua na ameshindwa kutatua matatizo yao.

Alisema jambo lingine ambalo limewadhihirishia dhahiri kwamba mwajiri wao anawabagua ni kushindwa kuwapatia fulana za kuvaa siku hiyo kama inavyokuwa miaka mingine ya nyuma, lakini mwaka huu, wamenyimwa fulana hizo badala yake wameambiwa labda watapewa fulana 200 tu, kati ya 6,000.

“Unajua mara nyingi serikali imeizoea kututumia katika mambo yao, lakini linapokuja suala la kudai madai yetu muhimu tunaonekana hatuna  umuhimu, kwa hiyo tumeona hakuna sababu ya kushiriki katika sherehe hizo maana hata fulana nazo wameshindwa kuzitoa,”alisema  Kihako.

Alisema walimu wa Sekondari hawataki kabisa kusikia suala hilo kwa kuwa walinyimwa  fedha za likizo, uhamisho na mambo mengine.

Kihako alisema  mpaka sasa  hawajalipwa fedha hizo na ni vigumu kumshirikisha mwalimu katika suala la Mei Mosi, mwalimu hawezi kukuelewa.

“Ebu fikiria mwalimu analia na njaa halafu inapotokea mambo ambayo sio muhimu kwake, ndiyo wa kwanza kuitwa, kwa hiyo tunapenda kumpa taarifa mwajiri kwamba hakuna mwalimu atakayeshiriki katika sherehe hizo,”alisisitiza Kihako.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo alisema tayari alikutana na uongozi  wa CWT na kwamba Manispaa yake imetoa Sh7 milioni kwa ajili ya suala hilo.

Fuime alisema kwa sasa Manispaa inakabiliwa na mambo mengi kama vile matatizo ya mafuriko na kwamba kuna baadhi ya barabara zinahitaji matengenezo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kama vile barabara ya Kivule na Kitunda zote zinahitaji matengenezo.

“Ni kweli nimepokea malalamiko hayo, lakini fedha zinazohitajika siyo chini ya Sh50 milioni, sasa kipi muhimu fulana za siku moja au kusaidia miradi ya maendeleo? Maana Manispaa inakabiliwa na matatizo mengi sana kwa hiyo hata CWT inaweza kutumia michango ya wanachama kusaidia walimu,  Manispaa ya Ilala imetoa Sh7 milioni,”alisema Fuime.

Alisema kwa kawaida vyama vingi ambavyo vina wafanyakazi wanatakiwa kutumia michango ya wafanyakazi kusaidia mambo mengine ambayo yanawahusu wanachama na kwamba CWT ilitakiwa kuchangia kutoka katika michango ya wanachama.

0 comments:

Post a Comment