Thursday, April 26, 2012

IMEDAIWA kuwa wahadhiri wengi  vyuo vikuu nchini wanakabiliwa na tatizo la kukumbwa na msongo wa mawazo  kuliko wafanyakazi wengine nchini.
Uafiti uliyofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuhusu msongo wa mawazo  kwa wafanyakazi mbalimbali nchini ulibaini kwamba wafanyakazi wa vyuo vikuu wako hatarini kukumbwa na tatizo hilo.
Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa ripoti ya utafiti huo, Mkuu wa Idara ya Elimu ya Saikolojia na Mitalaa, Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dk Kitila Mkumbo alisema kuwa utafiti umevihusisha vyuo vinne.
Vyuo vilivyohusishwa ni Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Chuo Kikuu cha Tumaini, Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo cha Mtakatifu John’s na kubaini wafanyakazi wanaofanya kazi katika vyuo hivyo wakiwa na tatizo hilo.
Dk Kitila alisema sababu kubwa zinazosababisha Wahadhiri kuwa na msongo wa mawazo ni kutokana na kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika na kwamba wengine wanashindwa kutimiza malengo yao kama vile machapisho ya kutosha kwa mwaka pamoja na matatizo ya wanafunzi.
Kutokana na hali hiyo, Dk Kitila alishauri waajiri kuwaandalia mazingira mazuri ya kufanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuwaajiri wanasaikolojia katika taasisi zao  ili kuweza kuwashauri waajiri na waajiriwa.
“Unajua sababu kubwa zinazowasababishia msongo wa mawazo wahadhiri wanafanya kazi nyingi sana,  mara nyingi wengine wanashindwa kuchapisha machapisho ya kutosha huku matatizo ya wanafunzi nayo yanakuwa mengi kama vile kushindwa kumaliza kazi wanazopewa,”alisema Dk Kitila.
Alisema kuwa wafanyakazi wengine wanakumbwa na msongo wa mawazo kutokana na kukosa vitendea kazi vya kutosha pamoja na migogoro kazini.
Alitoa wito kwa waajiri na waajiriwa kuepuka migogoro isiyo ya lazima kazini ili kuepuka mambo ambayo yanaweza kusababisha msongo wa mawazo hali inayosababisha mfanyakazi kufanya kazi vizuri.

0 comments:

Post a Comment