Thursday, April 26, 2012

Muungano wa Afrika umezitaka Sudan na Sudan Kusini kutekeleza mkataba wa amani kwa muundo mpya wa AU.
Baada ya kuwa kimya kwa muda, hatimae sauti ya Afrika inasikika kufuatia mzozo huo kati ya Sudan na Sudan kusini ambao sasa unatishia kuwa chanzo cha vita kati ya majirani hao.

Wajumbe wa baraza la usalama la umoja huo walimaliza kikao chao cha dharura kuhusu utata huo kwa kutoa maagizo mazito na kukariri njia ya kufuatwa ili kudhibiti hali mara moja.
Baada ya kupokea ripoti za wawakilishi wa serikali husika na hata mjumbe wa kamati maalum ya kuhusu utekelezaji wa mikataba ya amani kati ya nchi hizo, Umoja wa afrika umetaka pande zote mbili ziondoe majeshi yao katika mipaka hiyo inayo zozaniwa na wasitishe mashambulio mara moja.
Umoja huo pia umependekeza kuwa ujumbe maalum wa waangalizi wa mipaka pamoja na kikosi cha walinda amani cha umoja wa mataifa kitumwe katika maeneo hayo katika kipindi cha wiki moja ijayo.

Viongozi wa Sudan na Sudan kusini wametakiwa kuacha kutoa matamshi yanayochochea uhasama kati yao na kusambaza propaganda ambazo zinachochoea mzozo huo.
Baraza hilo la usalama ya Umoja wa Afrika pia limeamua kuunda kamati itakayo chunguza malalamishi kutoka pande zote mbili hizi na kubaini ukweli kamili kuhusu masuala wanayosema kuwa yanazua utata huo.
Pamoja na hilo serikali zote mbili zimeonywa dhidi ya kuwasiadia waasi walioko kwenye maeneo yanayozozaniwa.

Hili ndilo agizo kali zaidi kutolewa na umoja huo tangu mzozo huo uanze na umepata kuungwa mkono na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo pia lilikuwa na kikao chao jana.
Mwenyekiti wa baraza hilo balozi Susan Price kutoka Marekani, amesema kuwa hii ni hatua muhimu ya uongozi kutoka Afrika na kuwa baraza hilo halitasita kuchukulia serikali hizo hatua ikiwa zitapuuza maagizo hayo.

Kaluli hii imetolewa saa chache tuu baada ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, ambaye yuko ziarani nchini China kusema mashambulizi yaliotekelezwa na ndege ya kijeshi za sudan katika mipaka yao ni sawa na nchi hiyo kutangaza vita dhidi yao.
Kumekuwa na harakati chungu nzima za kidiplomasia kujaribu kuzuia vita kuzuka upya kati ya nchi hizi, na msukumo wa hivi karibuni umetoka kwa Rais Hu jing Tao wa China, ambaye amewataka viongozi hao wasitishe ugomvi huo.
Kauli ya Rais Hu Jing Tao ni muhimu sana kwa kuwa serikali yake inaushawishi mkubwa sana katika pande zote kwenye mzozo huo.

0 comments:

Post a Comment