Lema akipokea kadi za wanachama wapya simanjiro
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeendelea na
operesheni yake ya “Vua Gamba
Vaa Gwanda” ambapo juzi walifanikiwa
kuvuna zaidi ya wanachama 1,200 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka
maeneo mbalimbali ya wilaya ya Simanjiro.
Operesheni hiyo iliyoendeshwa kwa kutumia usafiri wa helkopta
(chopa) na magari iliongozwa na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho,
Godbless Lema akishirikiana na aliyekuwa mwenyekiti wa UV CCM mkoani
Arusha, James Olle Millya ambaye ni mwenyeji wa Simanjiro mwenye
ushawishi mkubwa kwa watu wa wilaya hiyo.
Wanaccm hao walirudisha kadi pamoja na sare mbalimbali za chama
hicho zikiwemo flana zilizokuwa na picha ya mwenyekiti wao wa Taifa,
Rais Jakaya Kikweta, bendera na vitambaa vya kichwa kwenye maeneo
ya Narekauo, Lolbosiret, Naberera, Ndovu, Orkesument na Marerani
ilikofanyika mikutano hiyo iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa watu.
Akizungumza kwenye mikutano hiyo Lema aliwataka wananchi kushiriki
kikamilifu kutoa maoni yao kwenye Tume ya Katiba pindi itakapopita
kwenye maeneo hayo ili kuhakikisha kero zao zinapatiwa ufumbuzi kupitia
katiba mpya ikiwemo kuhakikisha utitiri wa viongozi wasio na majukumu
kwenye mfumo wa serikali unaondolewa ikiwemo nafasi za wakuu wa wilaya
na mikoa ambao wanalipwa fedha nyingi huku wakiwa hawana kazi
wanayofanya zaidi ya kupeleka maneno “umbea” kwa viongozi wa juu.
Aidha alilitaka jeshi la polisi kumuhoji Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
kuhusiana na sakata la kutekwa Dk. Steven Ulimboka kwa kile alichodai
kuwa kunauwezekano akawa anawajua watekaji hasa kutokana na kauli
aliyoitoa bungeni siku moja kabla ya kiongozi huyo wa madaktari nchini
kutekwa na kuumizwa vibaya aliyosema kuwa liwalo na liwe.
Lema alisema kuwa jeshi la polisi linatakiwa kufanya kazi kwa
weledi likizingatia sheria hasa katika tukio hilo linalogusa hisia za
wengi na wapenda demokrasia kwani hakuna aliye juu ya sheria hivyo
waziri mkuu ahojiwe ili kuweza kubaini kilichokuwa nyuma ya kauli yake
hiyo.
Alisema kuwa ni vema mfumo wa kupata mawaziri ukabadilishwa kwa
watu kuandika barua za maombi badala ya sasa ambapo viongozi hao
hupatikana kwa kuteuliwa na rais miongoni mwa wabunge jambo linalopekea
utandaji wa serikali kuwa duni huku wananchi wakisidi kusongwa na kero
mbalimbali bila kupatiwa utatuzi.
Lema ambaye alikuwa mbunge wa Arusha Mjini kabla ya mahakama kumvua
mapema mwezi aprili mwaka huu, alishauri ni vema mfumo wa kuwapata
majaji nao ukaboreshwa kwa kuwepo na chombo cha kuwateua tofauti na sasa
ambapo huteuliwa na Rais wan chi jambo linalowafanya viongozi hao wa
muhimili wa kutoa haki kutokuwa huru.
Lema alitumia fursa hiyo kumshambulia mbunge wa jimbo hilo,
Christopher OleSendeka, (CCM), kuwa ni mtu asiye na msimamo huku
akimfananisha na tunda la tikiti maji ambalo nje ni kijani ndani ni
jekundu kwa madai kuwa mbunge huyo ni ndumila kuwili kwani mchana mbunge
huyo ni CCM lakini usiku hugeuka kuwa Chadema.
Alisema kuwa tabia hiyo ndiyo inayomfanya mbunge huyo wa Simanjiro
kushindwa kutetea maslahi ya wananchi wake ambao wengi wanaishi kwenye
lindi kubwa la umaskini ikiwemo kukosa huduma muhimu za barabara,
zahanati, elimu, afya na maji safi wakati jimbo hilo linahazina kubwa ya
utajiri ikiwemo machimbo ya madini yenye thamani kubwa ulimwenguni ya
Tanzanite.
“Asubuhi nimefanya mkutano kwenye kijiji cha Ndovu, nikaona
wananiletea chupa ya maji mwanzo nilidhani wananipa dawa lakini
nilisikitika wananchi wale waliponiambia maji hayo ndiyo wanayoyatumia
kwa ajili ya kunywa toka kwenye kisima wanachochangia na mifugo, hii ni
hatari sana kwa afya zao, ninawasiliana na wabunge wa Chadema ili
wayapeleke bungeni, hivi kwenye maisha haya yanawastahili wananchi
wanaoishi kwenye utajiri mkubwa wa Tanzanite?” alihoji Lema.
Kwa upande wake Millya aliwataka wananchi wa Simanjiro kuungana
naye kwa kuhamia Chadema ili waunganishe nguvu katika harakati ya kudai
haki zao ikiwemo kupigania kunufaika na madini ya Tanzanite
yanayopatikana ndani ya wilaya hiyo kwani CCM kwa miaka 50 imekuwa
ikitoa ahadi nyingi za neema kwa wananchi hao lakini hawazitekelezi.
Aliwataka wasitishike na vitisho wanavyotolewa na baadhi ya
viongozi wa CCM kwenye eneo hilo ambao wananchi walimweleza kuwa siku
moja kabla ya mkutano huo walipita kwenye kila boma(familia) wakiwataka
wananchi wasijitokeze kwenye mkutano huo lakini wananchi wakawapuuza na
kujitokeza kwa wingi.
Aliwataka wananchi hao kuwapuuza wale wote wanaojaribu kuwagawa kwa
kigezo cha wenyeji na wakuja kwa kile alichodai kuwa lengo la watu hao
siyo zuri kwani Watanzania wanahaki ya kuishi kwenye eneo lolote hapa
nchini hivyo waendelee kushirikiana katika kujiletea maendeleo na
kupigania haki zao kwa pamoja.
Millya alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa wakati Taifa
likifikisha miaka 50 ya uhuru lakini mpaka sasa wananchi wa jamii ya
kimaasai bado wananyanyaswa na kuwa kama ombaomba wa ardhi kutokana na
kutopewa ardhi ya kutosha kwa ajili ya shughuli zao za ufugaji na
makazi.
Viongozi wengine walihutubia kwenye mikutano hiyo ni pamoja na
aliyekuwa diwani wa Sombetini kwa tiketi ya CCM ambaye hivi karibuni
alihamia Chadema, Alphonce Mawazo na aliyekuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa
Taifa CCM na UVCCM, Ally Bananga.
habari kwa hisani ya habari Tanzania
0 comments:
Post a Comment