Yusuf Manji azua mjadala Yanga

WAKATI zoezi la kuchukua na kurejesha fomu za kuwania uongozi katika klabu ya Yanga likifungwa leo jioni, jina la aliyekuwa mfadhili wa klabu hiyo, Yusuf Manji, limekuwa gumzo kubwa.
Hiyo inatokana na hatua ya Manji kwenda makao makuu ya klabu hiyo juzi mchana na kutwaa fomu tatu za kuwania uongozi.

Kitendo hicho, kwanza kikatoa picha huenda Manji ameamua kuwania nafasi ya uongozi, wengine wakienda mbali, wakidai ameomba uenyekiti.
Licha ya Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo, Francis Kaswahili, kusema Manji amechukua fomu kwa niaba ya wengine, wengi wanasubiri orodha ya mwisho leo.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima kwa kuzungumza na baadhi ya wanachama, kwa kiasi kikubwa wamekuwa na maoni tofauti.
Wengine wanaona kitendo cha Manji kuwachukulia fomu wengine, ni kuwabeba wahusika kabla ya uchaguzi kutokana na ushawishi wake mkubwa ndani ya Yanga.

Hata hivyo, wengine wamekuwa na fikra kuwa Manji kama mwanachama wa klabu hiyo, anayo haki ya kufanya hivyo kwa mujibu wa katiba.
Aidha kuhusu hoja ya Manji kugombea au kutogombea, pia wanachama wamegawanyika, wengine wakifurahia na wengine wakiona hapana.
Kati ya wanachama wanaopinga Manji kugombea, ni Cyprian Msiba, Mussa Mfala, Shomari Mnola na Saidi Ngumba, wakisema Yanga haitatulia.
Aidha baadhi ya wanachama wanadhani kama Manji akijitosa kwenye uongozi, klabu hiyo itapiga hatua kiuchumi kutokana na uwezo wake kifedha.

Tanzania Daima ilipomtafuta Kaswahili jana jioni kuhusu Manji, alisisitiza kuwa hajachukua fomu kama mgombea, bali amewachukulia watu watatu.
Wakati uchukuaji na urejeshwaji wa fomu ukifungwa leo, wagombea jana walizidi kutokeza, lakini nafasi ya uenyekiti ikizidi kuogopwa.
Kati ya wanachama waliojitokeza jana, ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi, na Mkurugenzi, aliyeomba ujumbe kamati ya utendaji.
Wengine ni Yono Auction Mart, Stanley Kevela, nyota wa zamani wa timu hiyo Edger Fongo na Musa Katabalo, Mohamed Mbaraka, Auron Nyanda na Ally Mayay.
Alisema kufikia jana jioni, wanachama waliokuwa wamejitokeza walikuwa ni 21, huku uchukuaji na urejeshaji wa fomu, ukifungwa leo saa 10 jioni.
Hata hivyo, Kaswahili ametoa wito kwa wanawake wenye sifa na vigezo stahiki, kujitokeza kwani hadi sasa, wamekuwa kimya.
Ameonya kuwa baada ya kufungwa kwa muda huo wa kutoa na kurejesha fomu, hakutakuwa na nafasi tena ya kufanya hivyo.
Alisema nafasi ya mwenyekiti imeombwa na mmoja tu, John Jambele, huku nafasi ya makamu mwenyekiti ikiwaniwa na Ayoub Nyenzi na Isack Chenji.
Waliojitosa kwenye ujumbe ni Abdallah Sharia, Ahmed Gao, Lameck Nyambaya, Gaudensius Ishengoma, Peter Haroub, Ramadhan Kampira, Abdallah Bin Kleb, Muhingo Rweyemamu, Saleh Hassan na Jumanne Mwammenywa.
Uchaguzi huo unalenga kuziba nafasi za baadhi ya viongozi waliojiuzulu kwa shinikizo la wanachama wakiongozwa na baraza la wazee na kundi la vijana.
 http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=36707

0 comments:

Post a Comment