Friday, July 27, 2012

Kocha Mkuu wa Simba SC,  Milovan Cirkovic.
Na Mwandishi Wetu
WAKATI Simba ikiwa na wakati mgumu kutokana na timu yake kuonekana kushuka kiwango ikilinganishwa na msimu uliopita, Kocha Mkuu Milovan Cirkovic ameondoka nchini jana alfajiri kurejea kwao Serbia.
Uongozi wa Simba umesema Milovan ameondoka nchini kwa ajili ya kwenda kupumzika kwa muda halafu atarejea kuendelea na kazi.
Lakini mwenyewe amesisitiza ana mambo kadhaa ya kifamilia anayotakiwa kuyafanya katika kipindi hiki huku akisisitiza hataiathiri timu yake.
“Kweli ameondoka, atarejea nchini baada ya muda na moja kwa moja ataendelea kuinoa timu,” alisema jana asubuhi Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga.
 
Milovan ameiachia Simba programu ya kufanya na kusisitiza wachezaji wake wafanye mazoezi mepesi na wasicheze mechi yoyote ya kirafiki.
Kocha huyo amesisitiza hilo baada ya kugundua timu yake haikuwa na mazoezi ya kutosha, hali iliyosababisha ishindwe kufanya vizuri katika michuano ya Kagame na pia kusababisha majeruhi lukuki.
“Waendelee na mazoezi ya ndani (gym), angalau siku tano, baada ya hapo wanaweza kuendelea na mazoezi mepesi ya uwanjani. Nikirudi tutaendelea na programu nyingine,” alisema Milovan.
Kamwaga alisema watafuata programu hiyo. “Tunaifuata na Jumatatu tutaanza mazoezi mepesi ya uwanjani.”
Hata hivyo, hatua ya Milovan kuondoka ghafla, imewashtua baadhi ya Wanasimba kwa kuwa huu ndiyo ulikuwa wakati mwafaka wa kukijenga kikosi chake ambacho kimeonekana kina upungufu mwingi. Wiki chache zilizopita, kocha huyo alikuwa kwao Serbia na familia yake.

0 comments:

Post a Comment