WABUNGE vinara wa rushwa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM)
wametajwa na majina yao yako katika ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Tanzania Daima Jumatano limedokezwa.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya TAKUKURU kumnasa na kumfikisha
mahakamani Mbunge wa Bahi (CCM), Omary Badwel, kwa tuhuma ya kupokea
rushwa ya sh milioni moja kutoka kwa kiongozi wa serikali wa halmashauri
ya wilaya ya Mkuranga.
Habari ambazo gazeti hili imezipata, zilidai kuwa wabunge waliotajwa
ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)
ambao wanadaiwa kuwamo kwenye mpango wa kutaka kupokea rushwa kutoka
ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga.
Kamati ya LAAC inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP),
ina wajumbe 15, kati yao wajumbe watatu walipata kutajwa na Mbunge wa
Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR Mageuzi), katika Bunge la Bajeti
mwaka jana kwamba waliomba rushwa katika halmashauri ambayo hakuitaja.
Waliotajwa na Kafulila mwaka jana ni pamoja na Godfrey Zambi (Mbozi
Mashariki), Zabein Mhita (Kondoa Kusini) na Omar Badwel aliyefikishwa
mahakamani juzi kwa tuhuma za kuomba rushwa.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa TAKUKURU, Alex Mfungo, alipohojiwa
kuthibitisha taarifa hiyo hakukubali wala kukataa kuwapo kwa wabunge
wengine ndani ya kamati hiyo wanaotuhumiwa kwa rushwa.
Badwel alikamatwa na maofisa wa TAKUKURU katika Hoteli ya Peacock
jijini Dar es Salaam, akidaiwa kupokea rushwa kutoka kwa maafisa wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Akichangia Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano, Kafulila aliwataja
bungeni Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi na Mbunge wa Bahi,
Omary Badwel na Zabein Mhita wote wa CCM akidai kwamba aliwakuta
wakiomba rushwa kwa viongozi wa halmashauri.
Wakati akitaja majina hayo, Kafulila nusra aingie katika mgogoro na
aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge, George Simbachawene, ambaye alikuwa
akimwamuru kukaa chini kutokana na muda wake wa kuchangia kumalizika.
Hivi sasa Simbachawene ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
Kiti cha Spika kiliahidi kutoa mwongozo kuhusu tuhuma hizo, lakini
hadi sasa hakuna mwongozo uliotolewa kuhusiana na kauli ya Kafulila.
Bunge limechafuka
Wakati mbunge huyo akifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuomba
rushwa, hatua hiyo imeelezwa na wadadisi wa mambo ya siasa kwamba
imezidi kuuchafua muhimili huo wa dola.
Duru za kisiasa zinadai kuwa kashfa ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, David Jairo, ya kukusanya mamilioni ya fedha za
kuwapa wabunge ili wapitishe bajeti na hii ya Mbunge wa Kamati ya LAAC
kunaswa akiomba rushwa imeanza kupoteza heshima ya Bunge.
Kama hakuna kitakachofanyika kuzuia kasi hii basi jina la Bunge la
wala rushwa linaweza kuwa ndilo jina sahihi kwa taasisi hiyo.
Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa, amesema wabunge ndio wanaoongoza kwa rushwa na kutolea mfano wa kashfa ya Jairo.
“Ulisikia rushwa ilivyotembea wakati wa uchaguzi wa wabunge wa Afrika
Mashariki? Kamati ya LAAC imenaswa lakini naamini kuna kamati nyingi
zinafanya mchezo huo. Hii ni aibu kwa Bunge letu,” alisema Dovutwa.http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=36672
0 comments:
Post a Comment