• Ina vipaumbele saba, miundombinu ya kwanza
WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa, amesema makadirio
ya bajeti ya wizara kwa mwaka ujao wa fedha 2012/2013 yanatarajiwa kuwa
sh trilioni 15.
Hatua hiyo inaashiria kupanda kwa bajeti hiyo kwa trilioni mbili zaidi
ya bajeti ya mwaka unaomalizika 2011/2012 iliyokuwa na sh trilioni 13.
Jana Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi ilikutana na watendaji wa
ngazi za juu wa wizara hiyo kwa ajili ya kujadili mwelekeo wa bajeti kwa
mwaka ujao wa fedha.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Dk. Mgimwa ambaye
hiyo itakuwa bajeti yake ya kwanza tangu ateuliwe hivi karibuni kushika
wadhifa huo, alisema kuwa wizara yake imetoa vipaumbele saba huku cha
kwanza kikiwa sekta ya miundombinu.
“Ni kweli tumejadili kuhusu taarifa ya mwelekeo wa bajeti yetu na kwa
sasa makadirio tuliyonayo ni trilioni 15, ambapo katika miundombinu tuna
vipengele vine, ambapo ni lazima tuwe na umeme wa uhakika,
usafirishaji na uchukuzi, maji safi na salama pamoja na mawasiliano,”
alisema.
Dk. Mgimwa alitaja kipaumbele cha pili kuwa ni kilimo huku akieleza
kuwa maendeleo ya viwanda nayo wameyapa umuhimu na kuwa kipaumbele cha
nne.
Aliongeza kuwa pia maendeleo ya rasilimali watu wameyaangalia na kuona umuhimu wake.
“Utalii imekuwa kipaumbele namba tano, biashara za ndani na nje
tumeamua kuweka kiwe kipaumbele namba sita na kipaumbele cha saba ni
huduma za kifedha,” alisema Dk. Mgimwa.
Waziri huyo alisema kuwa hakukuwa na pingamizi katika makadirio ya
bajeti hiyo lakini alisisitiza ni vizuri kuwasiliana na Mwenyekiti wa
kamati hiyo, ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM)
ili kuweza kupata taarifa zaidi.
Hata hivyo Chenge hakuwa tayari kuzungumzia taarifa hiyo na kutoa
kauli fupi kuwa majadiliano bado yanaendelea, hivyo hawezi kuzungumzia
lolote juu ya jambo hilo.
Habari na na Betty Kangonga http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=36641
0 comments:
Post a Comment