WAKATI zoezi la uchukuaji fomu za kuwania uongozi wa klabu ya
Yanga likianza leo, Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), imefafanua kuwa ni uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi na si
uchaguzi mkuu.
Hatua hiyo, inatokana na baadhi ya wanachama wa klabu ya Yanga,
kukiuka kanuni hizo kwa kutoa taarifa potofu kuhusiana na uchaguzi mdogo
wa kuziba nafasi zilizowazi utakaofanyika Julai 15.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deogratius Lyatto, alisema
jijini Dar es Salaam jana kwamba uchaguzi huo ni kwa ajili ya kuziba
nafasi za viongozi ili kutimiza akidi na si kwa ajili ya kuchagua upya
viongozi kama inavyoenezwa.
“Kuna upotoshwaji unafanywa na baadhi ya wanachama kuhusiana na
uchaguzi huu, napenda ieleweke kuwa uchaguzi huo utajaza nafasi za
viongozi waliojiuzulu na ile ya mjumbe mmoja aliyefariki, hivyo
wanachama wa Yanga wafahamu hilo na kuzingatia,” alisema.
Mbali na hilo, mwenyekiti huyo alisema kwamba viongozi
watakaochaguliwa watakaa madarakani kwa muda uliosalia kama katiba
inavyoelekeza na kwa mantiki hiyo, watamaliza miaka yao minne mwaka
2014.
“TFF inaamini kuwa wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga,
watatekeleza wajibu na majukumu yao ya kikatiba na kikanuni, kuhakikisha
kwamba klabu hiyo inajaza nafasi zilizo wazi katika mkutano mkuu wa
uchaguzi kwa kipindi kilichobaki cha mamlaka ya kamati ya utendaji
(ibara ya 29 ya katiba ya Yanga),” alisema.
Kwa mujibu wa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, Francis
Kaswahili, zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu litamalizika Juni 6,
huku Juni 7 hadi 13 kamati itapitia majina ya walioomba kugombea na
kutangaza majina yao, wakati Juni 14 hadi 18 itakuwa ni kipindi cha
kupokea pingamizi.
Aidha Juni 19 hadi 23 utafanyika usaili na kutangaza matokeo, wakati
Juni 24 hadi 26 itakuwa ni kipindi cha kukata rufaa, Juni 27 hadi Julai
mosi Kamati ya Uchaguzi TFF itasikiliza rufaa kama zipo, huku Julai 2
yatatangazwa majina na kampeni kuanza hadi Julai 14.
Uchaguzi huo unatokana na kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti Lloyd
Nchunga, baada ya kushinikizwa na baadhi ya wanachama wakiongozwa na
Baraza la Wazee, kwa madai ya kushindwa kuiletea mafanikio chini ya
uongozi wake.
Pia nafasi zingine zitakazojazwa ni za Makamu Mwenyekiti iliyokuwa
inashikiliwa na Davis Mosha ambaye alijitoa miezi michache baada ya
kuchaguliwa, huku mjumbe Theonest Rutashoborwa akitangulia mbele ya
haki.
Uchaguzi huo pia utajaza nafasi za wajumbe walioachia ngazi ambao ni pamoja na Mzee Yusuf, Charles Mgondo na Ally Mayay.
Kwa sasa Yanga imebaki na wajumbe wanne, Mohammed Bhinda, Sarah
Ramadhan, Tito Osoro na Salum Rupia, ambao baada ya uchaguzi wataungana
na viongozi wapya na kuteua wajumbe wengine watatu kwa mujibu wa katiba,
hiyo inatokana na wajumbe hao wa kuteuliwa Seif Ahmed, Mbaraka Igangula
na Pascal Kihanga kujiuzulu.CHANZO http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=36572
0 comments:
Post a Comment