SHULE ya Sekondari ya Peace iliyoko Kata ya Kagondo, Manispaa ya
Bukoba, inayomilikiwa na Meya wa manispaa hiyo, Anatory Amani, imeingia
katika kashfa nzito ya kuwatapeli wanafunzi 84 wa kidato cha nne mwaka
2011.
Amani ambaye pia ni diwani wa kata hiyo, anadaiwa kuwahadaa wanafunzi
hao na kisha kuwahamishia shule nyingine ya Bernard ya wilayani Karagwe
kwenda kufanya mitihani yao ya mwisho kwa siri na kinyume cha sheria.
Kutokana na udanganyifu huo, Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA)
limeyafuta matokeo ya wanafunzi hao kwa kile kilichoelezwa kuwa majibu
yao yalikuwa na ufanano.
Uchunguzi wa Tanzania Daima ulibaini kuwa meya huyo alifanya ujanja
huo pasipo kuwashirikisha wazazi wa wanafunzi hao wala kufuata taratibu
za uhamisho wa Idara ya Elimu Mkoa wa Kagera.
Wazazi hao walidokezwa kuwa meya huyo amekuwa akiwachuja wanafunzi wa
kidato cha nne muda mfupi kabla ya mitihani ya mwisho na kubakiza wale
wenye uwezo mkubwa kimasomo ili shule yake ionekane inafaulisha zaidi,
hivyo kuwavutia wazazi.
Katika mahojiano na gazeti hili mjini Bukoba, baadhi ya wazazi hao
walieleza jinsi walivyopokea taarifa hizo kwa mshangao na masikitiko
makubwa na pia kusononeshwa na hatua ya meya huyo kukwepa kukutana nao.
Huku wakionesha orodha ya majina ya wanafunzi hao ambayo Tanzania
Daima ina nakala yake, walidai kuwa walilipa ada tangu kidato cha kwanza
hadi cha nne.
“Sisi tulishangazwa na hatua ya kutuambia kuwa tunapaswa kuchangia
gharama za watoto wetu kwenda Karagwe kufanya mtihani wao wa mwisho
katika sekondari ya Bernard, ikiwa ni siku moja kabla ya usajili
kufungwa,” walidai.
Mmoja wa wazazi hao, Fredson Rwegasira, ambaye ni mfanyabiashara
katika soko kuu la mjini Bukoba, alisema kuwa walipohoji ni kwanini
watoto wao wanahamishiwa Karagwe, walijibiwa kuwa hawakufikisha alama za
ufaulu na hivyo hawawezi kuendelea kubaki Sekondari ya Peace.
“Unajua meya anamiliki shule mbili hapa Bukoba ambazo ni Aman English
Medium Primary na Peace Sekondari, sisi wengine watoto wetu wamesoma
kwake toka chekechea, sasa iweje mwanafunzi afikie kidato cha nne ndipo
aambiwe hakufikisha alama za ufaulu?” alihoji Rwegasira.
Wazazi hao ambao wengi wao walionekana kuzungumza kwa jazba wakidai
watoto wao wameathiriwa kisaikolojia, walimlalamikia meya huyo wakidai
anawadharau na kuwapiga chenga.
Walibainisha kuwa walilazimishwa kuchangia sh 180,000 za kuwapeleka
Karagwe pamoja na kununua sare za shule ya Bernard, kama kituo cha
mitihani, lakini baada ya majibu kutoka, majina yao hayakuwa na matokeo.
“Jamani tumelipa sh milioni 1.5 kila mwaka ambayo hulipwa kwa awamu
tatu pamoja na sh 270,000 za masomo ya ziada, halafu leo unasikia
mwanafunzi kafutiwa mtihani,” alisema mzazi mmoja.
Kwamba hatua hiyo iliwalazimu kumfuata Ofisa Elimu wa Mkoa wa Kagera,
ambaye aliwaeleza kuwa watoto wao wamefutiwa matokeo, hivyo hawaruhusiwi
tena kufanya mitihani hadi baada ya miaka mitatu.
“Baada ya kumlalamikia ofisa elimu na kumweleza kilichotokea, naye
alishangaa maana hakuwa na taarifa za kuhamishwa kwa wanafunzi wetu
kutoka Peace kwenda Bernard,” walisema wazazi hao.
“Sisi tunahoji kama wanafunzi hawa wanarudia mtihani, nani atagharamia
maana mwenye shule tulikowakabidhi anatukimbia, kututisha, serikali
imekaa kimya, tufanyeje?” alihoji mzazi mwingine.
Alipotafutwa Ofisa Elimu wa Mkoa wa Kagera, Florian Kimoro, kutaka
kujua hatua zilizochukuliwa na ofisi yake dhidi ya mmiliki wa Shule ya
Peace, alionekana kukwepa.
“Siwezi kutoa ufafanuzi kwa mtu nisiyemuona, njoo ofisini kwangu
utapata ufafanuzi,” alijibu Kimoro na kukata simu yake ya kiganjani.
Hata hivyo baadaye alijibu kwa njia ya ujumbe mfupi akisema: “Taarifa
hizo sijazipata naomba uwasiliane na Ofisa Elimu wa manispaa kabla ya
kuja kwangu.
Meya Aman alipotafutwa alitoa majibu yenye utata ambapo licha ya
awali kukiri kumiliki shule hizo, baada ya kubanwa aligeuka na kukana
kuwa hana shule anayoimiliki nchini, huku akimlazimisha mwandishi aende
ofisini kwake apewe vielelezo.
Mwandishi alifika ofisini kwa meya mara mbili kama alivyotakiwa, ofisi
ilikuwa imefungwa muda wote na hata alipopigiwa simu na kutumiwa ujumbe
mfupi, hakujibu hadi leo.
na Edson Kamukara http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=36642
0 comments:
Post a Comment