MBUNGE wa Jimbo la Bahi, Omary Ahmed Badwel (CCM), jana
alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), akikabiliwa na
mashtaka mawili ya rushwa.
Mawakili wa TAKUKURU, Janeth Machullia na Ben Lincoln, walidai mbele
ya Hakimu Mkazi Faisal Kahamba kuwa mashtakiwa huyo katika kosa la
kwanza anadaiwa kupokea rushwa ya sh milioni moja kutoka kwa Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Jonathan Liana, kinyume na kifungu
cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya
mwaka 2007.
Ilidaiwa kuwa kati ya Mei 30 na Juni 2 mwaka huu katika maeneo tofauti
jijini Dar es Salaam, Badwel akiwa ni Mbunge wa Bahi na Mjumbe Kamati
ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na wakati huo akiwa ni ofisa wa
serikali kwa maana ya sheria ya TAKUKURU, alitenda kosa la kushawishi
ili apewe rushwa ya jumla ya sh milioni nane toka kwa Sipora Liana
ili kiasi cha fedha hizo azipeleke kwa wajumbe wenzake wa kamati hiyo
ya Bunge ili waweze kuipitisha ripoti ya fedha ya mwaka 2011/2012 ya
halmashauri hiyo.
Wakili Machullia alidai shtaka la pili ni kwamba kati ya Juni 2 mwaka
huu, katika Hoteli ya Peacock, mshtakiwa akiwa na nyadhifa zake zote
hizo alipokea rushwa ya sh milioni moja kutoka kwa Liana ili aweze
kwenda kuwashawishi wajumbe wa kamati hiyo ili waweze kuipitisha ripoti
ya fedha ya Halmashauri ya Mkuranga huku akijua kufanya hivyo ni kosa.
Hata hivyo mshtakiwa huyo anayetetewa na wakili wa kujitegemea Mpale
Mpoki alikanusha mashtaka yote na wakili wa Machullia alidai kuwa
upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Hakimu Mkazi Kahamba alikubali mbunge huyo kupewa dhamana kwa sharti
la kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao kila mmoja atasaini bondi
ya sh milioni nne na kusalimisha hati zao za kusafiria mahakamani,
sharti ambalo lilitimizwa na mshtakiwa huyo kupata dhamana ambapo kesi
hiyo imeahirishwa hadi Juni 18.
Kamati yakana kuhusika na tuhuma hizo
Katika hatua nyingine, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ya
Mtaa (LAAC) imesema kuwa isihusishwe kwa namna yoyote ile na mashtaka
yanayomkabili mwanakamati mwenzao, mbunge Badwel.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Idd Azzan alisema tuhuma
zinazomkabili Mbunge Badwel zinatokana na utashi wake binafsi na kwamba haihusiani na masuala ya kamati yao.
“Tumesikitishwa lakini nisema kila mtu atalipwa kwa kazi anayofanya na
kwamba sisi hatuyumbishwi na mtu mmoja na kamati yetu isihusishwe na
tatizo hilo,” alisema Azzan.
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=36640
0 comments:
Post a Comment