Tuesday, June 5, 2012

 •  Mzito mwingine Moshi ajiandaa kutimka
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekiliza tena Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuibomoa tena ngome yake baada ya kuwachomoa wanachama takriban 400, akiwamo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Kata ya Enduleni, Cosmas Lakani.
Lakani ambaye ni mmoja wa viongozi machachari na aliyekuwa tegemeo kubwa la umoja huo katika Wilaya ya Ngorongoro, alihama na wanachama 394 kutoka kata za Ngorongoro na Enduleni juzi na kufanya idadi ya Wana CCM waliojiunga na CHADEMA ndani ya miezi miwili kufikia 3,481.
Wanachama hao walihamia CHADEMA wakati wa mikutano ya hadhara iliyoongozwa na viongozi wa

CHADEMA Mkoa wa Arusha, akiwamo Mwenyekiti, Samson Mwigamba, kwenye kata hizo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa kadi ya CHADEMA, Lakani alisema kuwa amechukua hatua hiyo kwa vile serikali ya CCM imeshindwa kutatua kero za wananchi, na kibaya zaidi kuonekana kuwa wanathamini wanyama walioko katika mbuga kuliko watu.

Alizidi kuishambulia serikali akidai imeshindwa kuwapatia hospitali, ambapo kwa kipindi chote wamekuwa wakitegemea ile inayomilikiwa na Kanisa Katoliki, na kuhoji kama kanisa hilo lisingejitolea wao wangepata wapi huduma za afya.
Alidai kuwa amekuwa akizuiwa na uongozi wa juu kusema lolote kuhusiana na kero za wananchi, huku akitakiwa kufumba mdomo wake.
Baadhi ya wanachama hao walidai mbele ya viongozi wa CHADEMA Mkoa wa Arusha kuwa serikali imeshindwa kuwasaidia hata kupata chakula cha kutosha familia zao kama walivyowaahidi wakati wakiwazuia kuendesha kilimo cha kujikimu ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

“CCM imetunyonya mpaka mwisho, walisema tuache kilimo cha kujikimu watatupa chakula, lakini wanatupa chakula kidogo, wanaona mnyama anathamani kubwa kuliko sisi tunaoishi Ngorongoro. Ndiyo maana tunawaacha na CCM yao tumekuja CHADEMA itusaidie tukadai haki yetu,” alisema Ndaito Sabore.
Mwana CCM mwingine mpya wa CHADEMA, Shuraa Sungai, alisema kuwa CCM iliwadanganya kuwa itatoa ajira kwa vijana lakini inasikitisha mpaka sasa vijana wao wanahitimu kidato cha nne na wengine vyuo vikuu lakini wanarudi kijijini hapo baada ya kukosa kazi.
Mwenyeki wa CHADEMA wa mkoa, Mwigamba, aliwaeleza wananchi hao kuwa CCM haijawahi kuwa na sera ya kuwasaidia wafugaji, jambo alilosema limechangia kuibuka kwa mapigano kati ya wafugaji na wakulima mara kwa mara.

Naye mratibu wa Baraza la Wanawake Mkoa wa Arusha, Cecilian Ndossi na Ephata Nanyaro, walisema maisha ya wananchi hao yanasikitisha kwa vile wanaishi katika umaskini wa kupindukia wakati wilaya yao ikiliingizia taifa mamilioni ya fedha za kigeni kupitia utalii unaofanyika ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.
“Serikali ya CCM inaonesha ni kiasi gani inathamini wanyama kuliko wananchi wake, hata ukiangalia barabara zinazotumika kwa ajili ya utalii zimetengenezwa vizuri lakini hizi zinazokuja huku kwa wananchi ni mbovu na zinapitika kwa shida sana,” alisema Nanyaro.
“Mimi niko kwenye sekta ya utalii, Ngorongoro inaliingizia taifa mamilioni ya dola, Serikali ya CCM inaacha kuwaletea huduma muhimu kama hospitali, maji safi na barabara kwa sababu inajua nyie ni wateja wao, wakataeni mje CHADEMA tushirikiane kudai haki hiyo mpaka kieleweke,” alisema Ndossi.

Kada mwingine apasua vichwa viongozi wake huko Moshi, viongozi wa CCM wa Wilaya ya Moshi Vijijini, wanaumiza vichwa kujaribu kumzuia kwa kila mbinu kada wake maarufu, Ansi Mmasi, anayetajwa kuwa katika harakati za kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA.
Mmasi ambaye amekuwa mpinzani mkubwa wa mbunge wa sasa wa Jimbo la Moshi Vijijini, Dk. Cyril Chami, anatajwa kuwa miongoni mwa vigogo wa CCM ambao wanatazamiwa kukihama chama hicho, ili kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Moshi Vijijini, Gabriel Masenga, alidai kuwa hajapata taarifa rasmi kutoka kwa Mmasi kama anataka kuhama, lakini akakiri kusikia fununu hizo kupitia vyombo vya habari.

Mwenyekiti huyo amedai kuwa wao hawawezi kupuuza habari hizo kwa kuwa ni nzito, lakini akadai kuwa ikiwa itathibitika, itakilazimu CCM kupambana vilivyo kuhakikisha kuwa kinaweka mtu katika uchaguzi mkuu ujao anayekubalika katika jimbo ili lisiangukie mikononi mwa wapinzani.
Kumekuwapo na taarifa za kada huyo kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA kwa lengo la kuwania kiti cha ubunge katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2012 huku Mmasi mwenyewe akisita kuweka bayana msimamo wake.
Taarifa hizo zimewagawa wanachama wa CCM katika wilaya hiyo katika makundi mawili makubwa, huku wengi wao wakionya kuwa kuhama kwa Mmasi kutasababisha mpasuko mkubwa na huenda akafuatwa na kundi kubwa la wanachama.

Baadhi ya wanachama wa CCM waliliambia Tanzania Daima jana kuwa Mmasi ana nguvu kubwa za ushawishi wa kisiasa katika Jimbo la Moshi Vijijini licha ya kwamba aliangushwa katika kura za maoni katika uchaguzi mkuu mwaka 2010.
Mmasi hakukiri wala kukanusha taarifa za kuhamia CHADEMA, badala yake aliomba apewe muda wa kutafakari.http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=36639

0 comments:

Post a Comment