WAKATI Chama Cha Wananchi (CUF), kikiwaagiza wabunge wake
kuipinga bajeti ya serikali, serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa
imelazimika kuwatisha wabunge wake, ili waipitishe.
Hatua hiyo ya CUF inaelezwa imekitikisa zaidi chama tawala na serikali
yake ambayo sasa huenda italazimika kuifanyia mabadiliko makubwa bajeti
iliyosomwa Juni 14 mwaka huu ambayo imefikia sh trilioni 15 kutoka
trilioni 13.5 za mwaka 2011/2012.
Wachambuzi wa masuala ya siasa na uchumi wameweka wazi kuwa, kama
serikali haitokubali kubadilisha na kuongeza fedha kwenye miradi ya
maendeleo, itegemee kukwama kwa bajeti.
CCM kipo katika wakati mgumu hivi sasa kwa sababu tayari wabunge wake
wametangaza kuipinga, huku wengine wakiweka wazi kuwa ni afadhali
kufukuzwa chama kuliko kupitisha mambo yasiyo na masilahi kwa wananchi
waliowachagua.
Matokeo ya kupingwa kwa bajeti hiyo na vyama vya upinzani, wachumi na
wananchi wa kawaida, yamepata uzito mkubwa kufuatia kitendo cha
kujitokeza hadharani kwa baadhi ya wabunge wa CCM ambao wameanika kasoro
kubwa zilizomo, huku wakiishutumu serikali kwa kuandaa bajeti
iliyowasahau wananchi wa kipato cha chini.
Kujitokeza Alhamisi wiki hii, kwa Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM)
ambaye alifichua kukiukwa kwa makubaliano ya kuifanyia marekebisho
muhimu bajeti, na kufikia hatua ya kuapa kuwa ataipinga kwa nguvu zote
hata kama itamlazimu kufukuzwa ndani ya chama hicho.
Mpina alisema hawezi kuendelea kuwa mbunge wa CCM kwa hali hiyo, na
kwamba ni aibu kwake kuiunga mkono bajeti isiyolenga kumkomboa
mwananchi, huku ikiruhusu fedha nyingi kutumika katika mambo yasiyo ya
msingi.
Mbunge huyo ambaye amekuwa akitumia vielelezo kuweka uzito madai hayo,
anatoa mfano wa jinsi Wizara ya Nishati na Madini ilivyojitengea kiasi
cha zaidi ya sh milioni 567, kwa mawasiliano tu, badala ya sh milioni 72
ilizotumia mwaka jana.
Aliongeza kuwa, wizara hiyo imejitengea pia sh bilioni 2
zitakazotumiwa na kitengo cha mawasiliano na utawala, wakati mwaka jana
kilitumia sh milioni 53.87.
Wizara ya Fedha nayo inadaiwa kujitengea sh bilioni 1.456 kwa ajili ya
safari za ndani na nje ya nchi, wakati mwaka jana ilitumia sh milioni
815.
Hata hivyo, habari za kuaminika zimedai kuwa, Mpina hayuko peke yake,
bali kuna kundi kubwa la wabunge wa CCM nyuma yake, ambao wanamuunga
mkono na wameapa kuikwamisha bajeti, na ikishindana watatumia njia ya
kuzigomea na kuzikataa bajeti za wizara.
Habari zinadai kuwa, tayari uongozi wa juu wa CCM umeanza kuwafuatilia
kwa siri wabunge wake wanaoonekana kuwa wabishi, ili kujua wanapata
wapi ujasiri huo, huku kukiwa na hofu kuwa wanatumiwa na kundi moja la
viongozi ndani ya chama hicho, na wengine wakiwa mawakala wa vyama vya
upinzani.
Katika kile kilichoonekana kukabiliana na tishio hilo, juzi wabunge wa
CCM waliitwa chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na
kujifungia tangu saa 5:00 asubuhi hadi 12:30 jioni, ambapo inadaiwa
walilazimika kuipitia kikamilifu bajeti hiyo.
Katika kikao hicho, inadaiwa kuwa baadhi ya wabunge waliweka wazi
msimamo wao wa kuikataa bajeti hiyo, wakikosoa vifungu vingi na wengine
wakienda mbali zaidi wakidai kuwa serikali ilikuwa imewasaliti wabunge
na wananchi, kwa kutoa fedha kidogo katika shughuli za maendeleo.
Inadaiwa wabunge wengi walisema wataiunga mkono na kuipitisha, ikiwa
tu serikali itakubali kuifumua katika baadhi ya maeneo mengi na kupeleka
fedha nyingi katika shughuli za maendeleo.
Kikao hicho kilikuwa ni cha pili ambapo katika kikao cha kwanza,
wabunge wa CCM walitishwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwemo
kusimamishwa ama kuvuliwa uanachama, ikiwa wataendelea na msimamo wao wa
kupinga bajeti na kuwashambulia watendaji wa serikali.
Mashambulio hayo yalimwelemea zaidi Mbunge wa Mwibara, Kange Lugola,
ambaye mapema wiki hii, alisimama bungeni kuomba mwongozo wa Spika,
akimtaka aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo afute ama kuthibitisha
kauli yake kuwa wabunge wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC)
ilikuwa imehongwa.
Kange hata hivyo, alijaribu kujitetea huku akidai kutukanwa matusi ya
nguoni na Mkulo, jambo lililozidi kuchafua hali ya hewa ndani ya kikao
hicho, huku waziri huyo wa zamani aliapa kupambana na yeyote
anayeonekana kumsakama.
Habari zinasema kuwa, kama moja ya mbinu ya kuzima misimamo mikali ya
wabunge, Waziri wa Nchi, Utawala Bora, George Mkuchika, alisema sasa
atamshughulikia kikamilifu mbunge yeyote wa CCM atakayethubutu
kukwamisha mipango ya chama chao na serikali yake kwa kuwa anao uwezo
huo.
Wabunge wa CCM ambao mara kwa mara wamekuwa wakielezwa kutokubaliana
na uamuzi wa serikali ya chama chao, juzi walikwepa kuhudhuria kikao cha
wabunge wa chama hicho kwa lengo la kukwepa kufungwa midomo.
Hoja ya wabunge hao ni kwamba wanataka kuisulubu serikali yao bungeni,
ambako ndiko uwanja wao wa kujidai badala ya kuijadili kwenye kikao cha
chama.
CUF yaigomea bajeti
Chama cha Wananchi (CUF), jana kiliwaagiza wabunge wake kuipinga
bajeti hiyo, kwa kile walichodai ni ya kibangaizaji sambamba na kuwa
imeandaliwa kwa lengo la kuwadanganya wananchi.
Agizo hilo limetangazwa jana na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba, mbele ya wabunge wa chama hicho na waandishi wa habari,
alipokutana nao mjini hapa, akisema hawawezi kuunga mkono bajeti
aliyodai imejaa ubabaishaji na ni ya kisanii.
Lipumba alisema hawawezi kuunga mkono bajeti isiyowakwamua kabwela wa
Tanzania kutoka katika lindi la umasikini, na kuongeza kuwa hali ya
wananchi ni mbaya na mfumuko wa bei umeongezeka kutoka asilimia 10.9
mwaka jana hadi asilimia 18.
Apongeza utawala wa Mkapa
Profesa Lipumba aliushutumu uongozi wa Rais Jakaya Kikwete kwa
kuzembea katika nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, huku akimmwagia
sifa Rais wa zamani, Benjamin Mkapa.
“Tumefikishwa hapa na serikali hii isiyokuwa na nidhamu ya matumizi ya
fedha. Wakati wa utawala wa Mkapa, kulikuwa na udhibiti mkubwa wa
fedha, na alibana kiasi kwamba, hata waziri hakuruhusiwa kusafiri bila
kibali chake.
“Hali ya sasa ni ovyo, na umekuwa utawala wa Gezaulole, kila mtu anajifanyia atakalo,” alisema Lipumba.
Kiongozi huyo ambaye ni mtaalamu wa uchumi, alisema kumekuwa na
ongezeko kubwa la deni la taifa, matumizi mabaya ya fedha, na ahadi hewa
za kukamilisha mradi wa umeme wa megawati 60 ambao serikali imekuwa
ikiutolea maelezo kila mwaka.
Alifichua kuwa, serikali imemlipa mtaalamu wa kigeni dola milioni 40,
kutokana na mkopo wa dola milioni 400 kwa masharti ya kibiashara, na
ikaficha kuliweka jambo hilo katika kumbukumbu za vitabu.
“Awali tulikopa dola milioni 400 na gharama za mshauri ilikuwa dola
milioni 40 kabla ya riba. Hapa haikuelezwa gharama za kukopa, wala
haikusema, tumelijua hili baada ya kuona ripoti za Benki ya Dunia,”
alisema Lipumba.
CHADEMA kuitikisa zaidi
Wakati hali ikionekana kuiendea kombo Serikali ya CCM, macho na
masikio ya watu wengi kesho yataelekezwa katika hotuba ya kambi rasmi ya
upinzani inayoongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, ambaye pia ni Mbunge wa
Hai, Freeman Mbowe.
Tayari kambi hiyo imeshaweka wazi kuwa bajeti hii haijalenga kumkomboa
mwananchi, hivyo katika mazingira ya kawaida mjadala wke utakuwa mkali
zaidi
CHADEMA ambayo mara kwa mara imekuwa ikiwapa shida CCM kwenye mijadala
mbalimbali, sasa itaipasua zaidi bajeti kwa kuwa CUF na baadhi ya
wabunge wa chama tawala wameonekana kuangalia zaidi athari za bajeti
hiyo kwa wananchi.
Juzi, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema hotuba ya
bajeti imedhihirisha kuwa serikali iko taabani na haiwezi tena kuwa na
ujasiri wa kuongoza nchi.
Dk. Slaa alisema hatua ya serikali kutenga asilimia 70 ya fedha kwa
ajili ya matumizi ya kawaida na mengine yasiyokuwa ya lazima, huku
ikibakiza asilimia 30 tu katika matumizi ya maendeleo ambazo zaidi ya
nusu yake zitatokana na misaada na mikopo ya kigeni, ni ushahidi tosha
kuwa serikali haijali shida za watu.
Alisikitishwa na kuongezeka kwa deni la taifa, akidai kuwa
halimnufaishi hata kidogo mwananchi wa kawaida kwa kuwa zinaishia katika
mikono ya wajanja.
Habari na Charles Misango, Dodoma
0 comments:
Post a Comment