BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA)
limewataka wasomi nchini kutambua wajibu wao wa kulitumikia taifa, ikiwa
ni pamoja na kusimamia misingi iliyoachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere katika kuleta maendeleo ya nchi.
Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, John Heche, alitoa kauli hiyo jana
alipowahutubia wanachama wa chama hicho kutoka vyuo vya CBE na DIT
katika sherehe maalumu ya kufungua matawi ya CHADEMA katika vyuo hivyo,
iliyofanyika ukumbi wa Don Bosco jijini Dar es Salaam.
Alisema wasomi wengi wakiwa vyuoni mawazo yao yanalenga kuingia
ofisini na kuwa na nyumba bora za kuishi, bila kuwafikiria Watanzania
wanaotaabika katika lindi la umaskini, huku nchi ikiwa na rasilimali za
kutosha.
“Miaka miwili iliyopita nilikuwa kama ninyi katika harakati za vyuoni,
ninachoweza kuwasihi ni kwamba muepuke kukariri yaliyoandikwa na
wana-philosophia bila kufanyia kazi, kwa maana kama mtakuwa hamuwezi
kuwasemea Watanzania, basi elimu yenu itakuwa haina manufaa yoyote,”
alisema Heche.
Alisema ni aibu kwa wasomi wa Tanzania kufundishana namna ya kuomba
fedha kupitia miradi mbalimbali wanayoandika na kuwatafuta wafadhili wa
kuwapatia fedha, huku wakipishana na wafadhili hao wakiwa wamebeba
rasilimali za Tanzania na kuzinufaisha nchi zao.Akizungumzia bajeti ya
serikali iliyotangazwa hivi karibuni, Heche alisema ni aibu kwa nchi,
kwa kuwa asilimia kubwa inategemea utashi wa wafadhili, na kwamba
wakiamua kugoma kuisaidia nchi itakuwa imeshindwa kujiendesha.
Aliwasisitiza wanavyuo hao walioamua kuwa wanachama wa CHADEMA
wasihofu kuingia katika ulingo wa kugombea nafasi za uongozi wa nchi kwa
kile alichoeleza ukombozi wa kweli hauwezi kutoka kwa watu waliolelewa
katika fikra za CCM.
Alisema mfumo mbaya wa uongozi ndiyo unaompa rais madaraka ya kufanya
anavyojisikia, bila kujali hisia za wananchi na kutolea mfano uteuzi wa
Diodarus Kamala, Philip Marmo na Batilda Burhani kuwa mabalozi wa
Tanzania katika nchi mbalimbali, licha ya wananchi katika majimbo yao
kuwakataa kuwa hawafai kuwaongoza.
Aliongeza kuwa, katika mfumo huo huo wa uongozi usiojali hisia za
wananchi, ndipo wanapopatikana watoto ambao wazazi wao walikuwa katika
nafasi za uongozi katika serikali na chama, na wao leo ni viongozi wa
maeneo waliyaoacha wazazi wao.
“Mnawashuhudia leo kuna Nape Nauye, watoto wa mzee Kawawa na hata Adam
Malima, leo ndiyo viongozi wetu kama Tanzania hakuna watu wengine wa
kushika nafasi hizo,” alisema Heche.
Habari na Abdallah Khamis
0 comments:
Post a Comment