• Samatta, Kaseja waahidi vita
na Mwandishi maalum, Maputo
TIMU ya soka ya Tanzania, Kili Taifa Stars, leo inashuka dimbani
kuwakabili Msumbiji huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kim Poulsen, akisema
wana kibarua kigumu.
Licha ya ugumu huo, Poulsen alisema ushindi katika mechi hiyo ya kuwania nafasi ya kucheza fainali za Afrika, ni lazima.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Februari 29, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Mechi ya leo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto jijini hapa, inatarajiwa kuwa ya ushindani mkubwa.
Poulsen raia wa Denmark, alisema wachezaji wapo kwenye morali mkubwa wa kupigania ushindi.
“Msumbiji ni timu nzuri, wanacheza kwa kasi, lakini kila kitu
nimekifanyia kazi. Ninaamini tutafanya vizuri, kikubwa ni kufuata
maelekezo ya kila tunachopaswa kufanya,” alisema Poulsen.
Stars ilitua hapa Ijumaa na kufanya mazoezi juzi na jana.
Naye Nahodha wa Stars, Juma Kaseja alisema ana imani kubwa wataibuka na ushindi kwani kila mchezaji yuko fiti.
“Tunataka ushindi, tumejiandaa vilivyo, tunajua Msumbiji ni wazuri,
lakini wanafungika. Tuna ari kubwa ya kupigania ushindi,” alisema.
Mbwana Samatta, nyota wa kimataifa anayekipiga TP Mazembe ya DR Congo,
alisema Msumbiji wanastahili heshima yao, lakini wao wanataka kushinda.
“Tunawaheshimu Msumbuji, lakini hatuwahofii kiuchezaji, tunataka
ushindi. Tunajua bila ushindi tutakuwa kwenye nafasi mbaya, tutajitahidi
kadiri ya uwezo wetu tushinde,” alisema.
Katika hatua nyingine, Watanzania wanaoishi nchini hapa, wamekuwa na matumaini makubwa ya Stars kushinda mechi ya leo.
Anwar Aziz, Mohamed Abballah Na John Thomas wanaofanya shughuli zao mjini hapa, walisema wanaamini
Stars itashinda kwani Msumbiji haina makali kama zamani.
“Msumbiji ni timu nzuri kwenye kiungo na staili yao ya kucheza kwa
kasi. Kitu muhimu kwa Stars ni umakini, jamaa wanapiga sana mashuti,”
alisema Anwar.
Naye Salum Magimba anayeishi nchini hapa, alisema Stars iwe makini
kwenye safu ya ushambuliaji, na kamba Msumbiji si wazuri kwenye safu ya
ulinzi.
Watanzania wanaoishi hapa, wameahidi kujitokeza kwa wingi kuishangilia
Stars wakati wote katika mechi hiyo itakayoanza saa 10 jioni ya hapa,
sawa na saa 11 jioni ya Tanzania.
Mshindi wa mechi ya leo, atapangiwa kucheza na moja ya timu 16
zilizocheza fainali za Afrika Januari mwaka huu nchini Gabon na Guinea
ya Ikweta.
0 comments:
Post a Comment