Tuesday, May 22, 2012

USALAMA wa watoto ni haki inayopaswa kuhakikishwa na wazazi, walezi, walimu na jamii inayowazunguka katika maeneo mbalimbali wanamokuwa.

Wanapokuwa shuleni wanaangaliwa na walimu au walezi na wanapokuwa nyumbani wazazi,
walezi na ndugu ndio wanaowajibika moja kwa moja kuhakikisha usalama wao.

Jamii inayowazunguka nayo inahitaji kuona kuwa wako salama ingawa haishurutishwi kufanya hivyo, kama ilivyo kwa wazazi na ndugu wa familia.

Tanzania inaamini mtoto ni wa wote na kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha hadhuriwi na chochote, yeyote, mahali popote anapokuwa.

Lakini, imani hiyo inatoweka taratibu kutokana na ‘kuoza’ kwa roho za baadhi ya wanajamii
wanaothubutu kudhuru watoto kwa njia mbalimbali, pindi wanapohitaji msaada kutoka kwao.

Wanasahau kuwa wao ndio wanaotakiwa kuwa mstari wa mbele kuwasaidia na kuwalinda dhidi ya mabaya.

Nafahamu kuwa hilo si jambo geni na halishangazi tena. Wapo wanaowanajisi na wengine kuwalawiti wanapowakuta peke yao katika mazingira ambapo wangepaswa kuwapa msaada.

Tumesikia na kujionea kupitia televisheni madhara mbalimbali wayapatayo watoto kutokana na unyonge wao unaosababishwa na umri mdogo.

Baadhi yao wamekatishwa maisha, wapo walioondolewa viungo fulani katika miili yao na kufanyiwa unyama wa aina nyingine tofauti na tunaowaita wanajamii.

Aidha, kutokana na kuharibikiwa fikra, ushirikina na ugomvi usiokwisha ndani ya familia zetu, baadhi ya wazazi nao wamekuwa wakidhuru watoto wao badala ya kuwalinda.

Lakini, naamini kuwa yote hayo ni matokeo ya roho zisizomtii Mungu na kupuuza sheria. Hima turekebishe hali hii.

Nikiachilia mbali madhara hayo, napenda nizungumzie uzembe wa wazazi na walezi unaosababisha ajali za barabarani kwa watoto.

Nalenga maeneo yenye nyumba zisizo na nyua wala malango ambapo mtoto anaweza kutoka ndani na kukatiza barabara wakati wowote anapopata fursa ya kufanya hivyo. Ni hatari.

Wengi wanagongwa na magari kwa kutojua namna ya kujilinda na ajali. Umri wao mdogo ndio
unaochangia wasijue kama kuvuka barabara bila hadhari ni hatari, ndiyo maana nawakumbusha wazazi wapunguze pilika na kujali ulinzi wa watoto wao.

Kilichonisukuma kuandika waraka huu ni tukio nililoshuhudia hivi karibuni katika barabara inayopita katikati ya makazi ya watu kwenye eneo la Mwananyamala, Dar es Salaam.

Mtoto mwenye umri wa miezi tisa aligongwa na gari kwa bahati mbaya baada ya kukatiza ghafla barabarani akitokea upande alipokuwa mama yake.

Alikuwa akitambaa na wakati wote huo mama yake alikuwa akiuza karanga katika upande wa pili wa barabara ilipotokea ajali.

Mama alikuwa akiuza karanga na kumsahau mwanawe aliyemleta karibu na barabara. Kila aliyekuwa eneo lile alishikwa na butwaa kuona mzazi wa majeruhi yule akiendelea kuuza karanga hata aliposikia kuwa kuna ajali imetokea.

Hakushituka hadi waliomfahamu mwanawe walipomjulisha kilichotokea na kumfanya azimie.
Masikini, hakukusudia mwanawe agongwe lakini pilika zilifanya asahau kulinda usalama wake. Wapo wanaozembea na kuacha watoto wapite barabarani bila uangalizi.

Wanafanya hivyo huku wakifahamu kuwa hawajui namna ya kujiepusha na ajali. Kadhalika, unaweza kuona baadhi ya wazazi wakiacha watoto wa miaka chini ya mitano nje ya nyumba
baada ya saa tatu usiku kwa madai kuwa wanacheza na wenzao.

Wanawaacha bila kuwahakikishia usalama. Wazazi wengine wanawachekea watoto wao wanaotoka nyumbani alfajiri na kwenda kuendesha matairi barabarani.

Tena wanatoka wakiwa vifua wazi na wakati mwingine hawavai viatu. Watoto kama hao ni lazima waufurahie uhuru huo kwa sababu hawajui hatari yake.

Kwa umri wao, wanaona ufahari kuranda bila hadhari. Wazazi nao kwa sababu ya shughuli nyingi wanaona uwepo wa watoto hao kuwa kero na hivyo kuwaachia wajiendee watakapo.

Hiyo si sahihi. Wajibikeni kuhakikisha wako salama wakati wote.

0 comments:

Post a Comment