Polisi
jana walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi wa
vyuo vikuu vya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo cha Elimu ya Biashara
(CBE) na St. John's tawi la Dar es Salaam waliokwenda Bodi ya Mikopo ya
Elimu ya Juu (HESLB), kufuatilia mikopo yao.
Hata
hivyo, bodi hiyo imesema kwamba akaunti yake ambayo inaitumia kulipa
mikopo ya wanafunzi "inasoma ziro" na kwamba hatua hiyo inasababisha
ishindwe kuendelea kutoa huduma.
Kauli
hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi mtendaji wa bodi
hiyo, George Nyatega alipozungumza na wanafunzi hao waliovamia bodi
hiyo kumshinikiza iwalipe fedha za ada, utafiti pamoja na chakula.
Licha
ya kutoa kauli hiyo, wanafunzi hawakukubaliana naye na badala yake
waliendelea kushinikiza walipwe fedha ndiyo waondoke. ''Sisi tunaamini
kwamba bodi hii ina fedha na inazitafuna huku ikishindwa kutulipa sisi
hivyo hatutoki hapa mpaka tupate fedha zetu,'' walisema wanafunzi hao
mbele ya Nyatega.
Baada
ya majibishano ya saa kadhaa bila suluhu uongozi wa bodi ya mikopo
ulilazimika kuita jeshi la polisi ili lisaidie kuwaondoa wanafunzi hao
ambao walikuwa wakipiga kelele na kusema kwamba hawaondoki hapo mpaka
walipwe fedha hizo.
Muda mfupi magari ya polisi yaliyokuwa na askari waliovalia sare na wengine nguo za kiraia yalifika katika ofisi hizo na kuwakuta wanafunzi hao wakiendelea kupiga kelele na kuwataka waondoke mara moja.
Hata
hivyo, wanafunzi hao walikaidi mpaka polisi walipoanza kufyatua mabomu
ya machozi ili kuwatawanya ambapo baada ya kuona imekuwa ngumu walianza
kukimbia hovyo huku na kule.
Wanafunzi hao baada ya kuona hali imebadilika na mabomu yameanza kupigwa walianza kutimua mbio lakini hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na tukio hilo wala kujeruhiwa.
Akizungumza
kabla ya kupigwa mabomu mmoja wa wanafunzi hao kutoka Chuo cha St.
John's, Nuru Karua, alisema fedha wanazodai ni mkopo na wanajua
watazilipa lakini hajui ni kwani nini serikali imekuwa ikiwazungusha.
Awali,
Nyatega alisema ofisi yake imeshaandaa malipo yote kwa ajili ya
kuwalipa wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya elimu ya juu lakini inashindwa
kupeleka hundi za malipo benki kwa kuwa haina hata shilingi moja.
"Akaunti yetu ya bodi ya mikopo haina kitu ndugu wanafunzi kwa kuwa Hazina yaani serikali haijatupatia fedha sasa sisi tutawalipa kitu gani hata kama mmekuja hapa kudai fedha hizo,” alihoji Nyatega.
Alisema bodi imeshawalisha taarifa kwa Hazina kuomba fedha hizo na kwamba wamejibiwa watapatiwa wiki hii muda wowote na kuwataka wanafunzi hao kukubalina na kauli yake.
Kufuatia
ukata huo, Nyatega alisema vyuo vilivyolipwa mpaka sasa ni Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Ardhi (Aru) na Chuo cha
Usimamizi wa Fedha (IFM).
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alipotafutwa kwa njia ya
simu jana kuelezea tukio hilo hakutapatikana baada ya msaidizi wake
kupokea simu muda wote na kusema alikuwa kwenye kikao kwa siku nzima.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment